NA MWANAJUMA MMANGA

VIKUNDI vya ushirika 12 Wadi ya Kipungani, vimekabidhiwa shilingi milioni 12, na kutakiwa kufungua akaunti za benki ,ili kuepusha upotevu wa pesa  zinazozalishwa kupitia  mitaji yao.

Diwani wa Wadi ya Kipungani, ambae pia ni Mstahiki Meya wa baraza la Manispaa Magharibi ‘B’ Khamis Hassan Haji, aliyasema hayo wakati wa  kukabidhi hizo kwa makatibu wa vikundi hivyo vilivyomo ndani ya wadi hiyo.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina dhamira  ya kuwasaidia wajasiriamali kupitia vikundi vya ushirika, hivyo ni vyema kuweka utaratibu wa kufungua akaunti zitakazorahisisha upokeaji wa misaada ya fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo.

Alisema vyama vya ushirika vina nafasi kubwa ya kuwasaidia wanachama wake katika kuwapatia mikopo, ili kuanzisha miradi kuweza kujiajiri wenyewe.

Alisema kufanya hivyo kutaweza kujikomboa na hali ngumu ya umaskini.

“Tutapowapa mitaji wachama wetu tutaweza kuwasaidia kujiajiri pamoja na kukabiliana na hali ngumu za kimaisha”alisema Mstahiki Meya huyo.

Hivyo aliwaomba wanachama hao kulipa mikopo kwa wakati kwa wale walipatiwa ili kuweza kuwasadia wenzao.

Nae Ofisa Uhusiano kutoka Benki ya NMB tawi la Zanzibar, Juhudi Kihamaya, alisema vikundi vya ushirika vina fursa  ya kupata mikopo ya  kuendesha vikundi vyao hivyo aliwasihi  kutumia fursa hiyo, ili kuviinua vikundi vyao  kimaendeleo.