NA KHAMIS MOHAMMED
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais, Dk. Sada Mkuya Salum, amesema kuwa sensa ya watu na makaazi inasaidia kupata takwimu sahihi kwa ajili ya kutunga sera na kupanga mipango ya maendeleo
Aliyasema hayo jana wakati akifungua mkutano wa wadau mbalimbali waliokua wakijadili dodoso la sense la mwaka 2020/2022 katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakili, Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Alisema, matumizi ya takwimu ni muhimu katika mipango ya serikali, ndiyo maana nchi imekua ikifanya sensa kwa muda uliopangwa bila ya kukosa kutokana na umuhimu wake.
Alisema, serikali itahakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi mkubwa na sensa ya mwaka 2022 ni ya tofauti ukilinganisha na sensa zilizopita.
Alieleza kuwa upatikanaji wa takwimu zinatazotokana na sensa zitatumika kupima mafanikio ya dira na mipango ya maendeleo.
“Tunawashukuru sana wadau wa maendeleo kwa kuendelea kushirikiana na serikali kutusaidia kuona kwamba hili zoezi ni muhimu kwa ajili ya utekelezaji wa maendeleo”, alisema, Dk. Mkuya.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Mayasa Mahfoudh Mwinyi, alisema, wameamua kujadili dodoso la sensa hilo ili kufanya maandalizi mapema ambapo sensa ya mwaka 2022 itakua ni ya kipekee ilikinganishwa na sensa zilizopita.
“Sensa ya 2022 itakua ni yakipee kwa sababu ni ya kidigitali itakayowezesha kupata matokeo kwa muda mfupi na kupunguza gharama”, alisema.
Alisema kuwa sensa hiyo kwa mara ya kwanza itawezesha kupata takwimu na viashiria mbalimbali vya kiuchumi na kijamii hadi ngazi ya shehia kulingana na sensa iliyopita ambayo ingeruhusu kutoa takwimu katika ngazi za wilaya.
“Sense ni takwa la kisheria na inafanyika kwa kufuata mpango maalum hivyo hadi sasa mbali ya hatua ya kujadili tunaendelea kukamilisha miongozo mbalimbali ya kusaidia watu.
“Maandalizi mengine ni kufanya majaribio mwaka huu, kutoa mafunzo kwa watumishi mbalimbali wakiwemo wadadisi na wasimamizi”.