NA ABOUD MAHMOUD

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum, amewataka watendaji wa masuala ya mazingira na mabaraza ya miji kukaa na kuandaa mpango utakaowawezesha kupatikana kwa nyenzo za kufanyia kazi ili kuweka miji katika hali ya usafi.

Aliyasema hayo wakati alipokutana na watendaji hao pamoja na ujumbe wa watendaji wa baraza la jiji juu ya kutafuta namna bora ya kuimarisha usafi wa mji huko Ofisini kwake Migombani nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Alisema mbali na hayo ni vyema kuwajengea uwezo wa kitaaluma wahusika ili waweze kufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kuweka jiji la Zanzibar kuwa safi.

“Ushauri wangu kwenu ni kukaa pamoja baina ya watendaji wote wa masuala ya mazingira pamoja na watendaji wa mabaraza za miji kuhakikisha wanaandaa mpango ambao utasaidia kupatikana kwa fedha za kutafuta nyenzo za kufanyia kazi,”alisema.

Waziri huyo alisema kwa sasa kuna umuhimu wa wadau hao kufanya kazi kwa pamoja ili kuona maagizo ya viongozi juu ya kuweka mazingira safi katika maeneo yote ya miji yanaimarika hivyo katika kufikia hatua hiyo kunahitajika mipango mbali mbali ikiwemo fedha na vitendea kazi stahiki kwa ajili ya kuimarisha eneo kuu la kutupia taka.

Alieleza kwamba bila ya kuwepo kwa mashirikiano kati ya taasisi hizo maendeleo hayatoweza kupatikana na wala mji hautokuwa safi, hivyo ni vyema kwa taasisi hizo kuzidisha mashirikiano ambayo yatasaidia jiji kuwa safi.

Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar, Mstahiki Mahmoud Mohammed Mussa, alisema watendaji wa mabaraza hayo wana kila sababu ya kujifunza jinsi ya kuimarisha huduma za usafi wa miji kupitia miji iliyopiga hatua.

Alisema kuwepo kwa usafi katika jiji la Zanzibar ni vizuri kwani ni jambo litakalohamasisha watalii wengi kutoka mataifa mbali mbali  kutembelea Zanzibar na Serikali kufikia kukuza uchumi wake kupitia sekta hiyo.

“Ni vyema kuiga mfano kwa miji kama Tanga, Arusha na Rwanda kutokana na usafi wa miji yao naamini kama na sisi tutafanya hivyo na jiji letu litakua safi watalii wengi kutoka mataifa mbali mbali wataweza kufika kwa wingi na Serikali itakuza uchumi wake,” alisema.