Miradi ya barabara, maji, elimu kukamilishwa

NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi wa shehiya ya Kiongwe kuwa barabara ya Bumbwini – Kiongwe, itajengwa kwa kiwango cha lami na kukamilika katika kipindi kifupi kijacho.

Dk. Mwinyi alitoa ahadi hiyo jana alipozungumza na wananchi wa shehiya ya Kiongwe na vijiji jirani, baada ya kutembelea na kukaguwa matayarisho ya mradi wa barabara ya Bumbwini hadi Kiongwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja, sambamba na mradi wa upelekaji umeme na maji safi na salama.

Alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 7.8 inayoanzia Bumbini hadi Kiongwe itajengwa kwa kiwango cha lami, ambapo matayarisho ya msingi ya ujenzi huo yakiwa yamekamilika.

Dk. Mwinyi alisema kila binadamu anahitaji maji, ikiwa sehemu ya maisha yake, hivyo akaahidi kusimamia uwekaji wa mabomba kwa wastani wa kilomita tano, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha huduma hiyo muhimu inapatikana kijijini hapo.

Aliiagiza wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kujenga madarasa sita yanayohitajiwa na wananchi wa shehiya hiyo ili kuwawezesha wanafunzi wa skuli iliopo kijijini hapo kupata huduma za elimu kwa ufanisi.

Aidha, aliwahakikishia wananchi wa shehiya hiyo kuwa serikali itatoa unafuu katika kuwaunganishia umeme, huku matayarisho ya kazi hiyo ikiwa katika hatuza za mwisho kukamilika.

Alilitaka Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kuhakikisha kijiji jirani na Shehiya hiyo nacho kinapatiwa huduma za umeme ili wananchi wake waweze kunufaika na huduma hiyo.

Dk. Mwinyi alikiri kuwa wavuvi wa Zanzibar ikiwemo wa kijiji cha Kiongwe wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa vifaa vya kisasa vya uvuvi, hivyo kuendelea kutumia vifaa duni na kushindwa kufikia malengo yao na akabainisha mikakati ya serikali katika kuleta mageuzi ndani ya sekta hiyo.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi aliwahakikishia wananchi wa Shehiya ya Donge Chechele kuwa barabara ya Donge Mbiji hadi Chechele yenye urefu wa kilomita mbili itajengwa kwa kiwango cha Lami, pamoja na kulijenga daraja liliopo ili kuwawezesha wananchi kusafirisha bidhaa zao kutoka mashambani na hivyo kuchochea shughuliza kiuchumi.