Asema utaimarisha uwekezaji

RAJAB MKASABA, IKULU ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameunga mkono mashirikiano yanayoimarishwa kati ya Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika suala zima la kuimarisha uwekezaji nchini.

Dk. Mwinyi ametoa baraka wakati wa mazungumzo aliyoyafanya kati yake na uongozi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) chini ya  Mkurugenzi Mtendaji wake Shariff Ali Shariff pamoja na uongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake Dk. Maduhu Isaac Kazi, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu jijini Zanzibar.

Dk. Mwinyi alisema kuwa jambo wanalolifanya na kuendeleza utaratibu wa kukuza mashirikiano ni jambo la busara na lina tija kubwa katika masuala ya uwekezaji hapa nchini kwani fursa zilizopo zinafaa kufanywa kwa pamoja.

Alieleza kuwa ipo haja ya kuimarishwa zaidi Hati ya Maelewano (MOU) iliyokuwepo awali kwani wakati umefika kwa mambo yaliyokuwa hayamo kuingizwa  kwa lengo la kupata tija zaidi kwa pande zote mbili.

Alisema kuwa suala la kubadilishana uzoefu kati ya taasisi hizo ni jambo muhimu sana hatua ambayo itasaidia kupatikana kwa mafunzo kwa watendaji wa Taasisi hizo kwa azma ya kuimarisha sekta ya uwekezaji hapa nchini.

Aidha, alieleza ndoto yake ya kuona kwamba Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) inakuwa na Kituo Kimoja cha Kutoa Huduma ili kuondosha urasimu na ucheweleshaji wa kutoa huduma kwa wawekezaji na kuifanya sekta hiyo kuwa rahisi hapa nchini.

Hivyo, Dk. Mwinyi amezishajihisha taasisi hizo na kuzitaka kuwa kioo na kielelezo thabiti katika kuhakikisha suala zima la uwekezaji linaleta manufaa kwa Taifa.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA,  Shariff Ali Shariff, alieleza kwamba mashirikiano yanayoimarishwa kati ya taasisi mbili hizo ni njia mojawapo ya kuimarisha muungano uliopo hasa ikizingatiwa kwamba taasisi hizo zinategemeana.

Alisema kuwa mashirikiano hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza sekta ya uwekezaji hapa nchini na kueleza kwamba ziara ya siku tatu ya Taasisi ya (TIC) hapa Zanzibar ina azma ya kuangalia maeneo ya kushirikiana kwa lengo la kuitangaza Zanzibar.