Asema utanuzi unaakisi malengo

NA KASSIM ABDI, OMPR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema uwepo wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere visiwani Zanzibar ni kielelezo chanya katika kuenzi na kudumisha kwa vitendo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Dk. Mwinyi alieleza hayo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa chuo hicho kampasi ya Karume, Zanzibar.

Alieleza kuwa uongozi wa chuo hicho umefanya kazi nzuri tangu kuanzishwa mwaka 1961 kulikopelekea kuendelea kuwepo hadi sasa kama yalivyo mawazo ya waasisi wa Taifa hili, marehemu Mwalimu Julius Nyerere na marehemu Sheikh Abeid Amani Karume.

Alisema kutokana na jitihada zinazochukuliwa na uongozi wa chuo hicho, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatambua mchango unaotolewa na chuo hicho katika kutoa mafunzo ya ngazi mbalimbali.

Alieleza kuwa chuo kina mchango katika kutoa mafunzo ya uongozi, maadili na uzalendo kwa wanafunzi na watumishi ambao kwa namna moja au nyengine wanasaidia katika kutekeleza majukumu yao kupitia serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Alifafanua kuwa, wahitimu wanaotoka katika chuo hicho wana mchango mkubwa katika ufanisi wa kazi kwa kuwa huwa wameiva, wenye uadilifu na weledi jambo ambalo lina umuhimu kwa watu wanaopewa dhamana katika utumishi wa umma.

“Tangu kuanzishwa kwa chuo hiki kimewanufaisha watanzania wengi na serikali kwa ujumla, kupitia chuo hichi kimepata wahitimu wengi wenye ari na bidii ya kulitumikia taifa hili kwa uweledi na kuchangia katika maendeleo ya taifa,” alieleza Makamu wa Pili wa Rais kwa niaba ya Rais Mwinyi.

Alisema kitendo cha chuo hicho kuanzisha ujenzi wa mabweni ya wanafunzi kinaashiria kutekeleza kwa vitendo mipango ya serikali ya awamu ya sita kwa kuzingatia maelekezo mbali mbali ya serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ikiwemo suala la kuongeza udahili wa wanafunzi na ujenzi wa miundombinu mbali mbali katika taasisi za Kielimu.