NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, amefanya uteuzi wa Makatibu wakuu na Manaibu pamoja na kuwatengua baadhi ya wakurugenzi katika wizara za serikali ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Ahmeid Said, alisema Dk. Mwinyi amemteuwa Mussa Haji Ali kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu.

Wengine aliowateuwa ni Issa Mahfoudh Haji kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ na Habiba Hassan Omar, atakuwa ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji.

Wengine ni Aboud Hassan Mwinyi, aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango anaeshughulikia (Fedha na Mipango) na Mikidadi Mbarouk Mzee, ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mhandisi Zena, uteuzi huo umeanza jana na wataapishwa kesho asubuhi saa 4:00 Ikulu Zanzibar.

Aidha waliotenguliwa ni Dk. Fadhil Mohammed Abdulla, aliyekuwa Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya, Ramadhan Khamis Juma aliekuwa Mkurugenzi Utumishi na Uendeshaji katika Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto.

Wengine ni katika Wizara ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, aliekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Magharibi ‘B’, Ali Said Natepe na Makame Mwadini Silima, aliyekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Mji Kaskazini ‘B’.

Wengine waliotenguliwa uteuzi wao ni Muhamed Salum Muhamed, aliekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Mji Kati, Kassim Mtoro Abu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kusini Unguja.

Alisema katika Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, alisema Dk. Mwinyi, amemtengua, Abdulhamid Idrissa Haji, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Wakala wa Maendeleo ya Viwanda Vidogo vidogo na vya Kati (SMIDA).