Aahidi ushirikiano kuinua tasnia ya filamu,utamaduni

NA MWINYIMVUA NZUKWI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuimarisha sekta ya utalii na utamaduni nchini.

Alieleza hayo juzi usiku katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya mtandao  ya uzinduzi wa tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF), uliofanyika Ngome Kongwe, Zanzibar.

Alisema tamasha hilo kama yalivyo matamasha mengine ya ndani na nje ya nchi, limechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi na ukuaji wa uchumi.

Hivyo Dk. Mwinyi alizitaka Wizara za Utalii na Mambo ya Kale na Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana, Utamaduni na Michezo, kufanya kazi kwa karibu na waandaaji wa matamasha hayo, ili yaendelee kuongeza tija katika maendeleo ya nchi na watu wake.

Aliongeza kuwa kuwepo kwa tamasha hilo kumechochea ongezeko na mwamko wa watu, wanaoangalia na kuandaa filamu za ndani jambo linaloimarisha utamaduni lakini pia kuongeza ajira.

“Kwa hakika napata matumaini makubwa kuona namna sekta binafsi inavyoendelea kushikiana na serikali. Kwa pamoja tumeweza kuandaa mashindano ya kimataifa ya riadha na tumeamua kuwa tamasha hilo lifanyike kila mwaka hivyo nawalikeni nyote kushiriki kila mwaka,” alieleza Dk. Mwinyi.