NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, leo atakuwa miongoni mwa wakimbiaji wa marathoni ya kimataifa Zanzibar (ZIM) itakayoanzia katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Mbio hizo zinazofanyika nchini baada ya zaidi ya miaka 10 kupita, inatarajia kushirikisha viongozi na wanamichezo kutoka ndani na nje ya Zanzibar, zitapita katika maeneo na mitaa ya mkoa wa Mjini Magharibi.

Kwa mujibu wa waandaaji wa marathoni hiyo, mbio hizo zitakuwa katika umbali wa kilomita 21, kilomita 10, kilomita 5 na mita 700 kwa watoto.

Akitaja njia za mbio hizo katika moja ya mikutano na wandishi wa habari wakati wa maandalizi yam bio hizo, mshauri wa ufundi wa kamati ya maandalizi Joshua kayombo ‘Joka’, alieleza kuwa mbio za kilomita 21 zitaanzia katika uwanja wa amani na kupita kaika mitaa mbali mbali kabla ya kumalizia uwanjani hapo wakati mbio za kilomita 5 zitaanzia ngome kongwe.

“Kama ilivyo moja ya lengo ya mbio hizi ni kutangaza vivutio vya utalii, katika mbio za kilomita 21, 10 na tano mbali ya kupita katika mitaa ya unguja mjini, pia watapita mji mkongwe,” alieleza ‘Joka’.

Alieleza kuwa katika maeneo yote kutakuwa na waongozaji, wasaidizi pamoja na viburudishaji kwa ajili ya wakimbiaji huku akiwahakikishia wakimbiaji hao kuwa njia zote zitakuwa na usalama wa kutosha.

Mbio za kimataifa za marathoni ya kimataifa ya Zanzibar (ZIM) imeratibiwa kwa pamoja kati ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kamati maalum yam bio hizo inayoongozwa na Hassan Zanga, zimelenga kurejesha mashindano hayo kwa lengo la kuhamasisha michezo yote ukiwemo wa marathoni na utalii kupitia sekta ya uchumi wa Buluu.