NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza umuhimu kwa nchi za Afrika kushirikiana katika kuimarisha sekta ya biashara.

Dk. Mwinyi alieleza hayo jana ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ethiopia nchini Tanzania Yonas Yosef Sanbe ambaye alifika ikulu kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais.

Katika mazungumzo hayo, alimueleza balozi huyo kuwa nchi za Afrika zina kila sababu ya kushirikiana katika kuimarisha sekta ya biashara hasa ikizingatiwa kwamba zina rasilimali za kutosha.

Dk. Mwinyi alimueleza balozi huyo wa Ethiopia kuwa Zanzibar inathamini ushirikiano wa uhusiano wa kihistoria uliopo baina ya Ethiopia na Tanzania na kumuhakikishia kwamba hatua hiyo itaendelezwa kwa azma ya kuimarisha maendeleo.

Alimueleza Balozi Sanbe kwamba kuwepo kwa safari za kampuni ya ndege ya Ethiopia katika nchi nyingi za bara la Afrika ikiwemo Tanzania kutauimarisha zaidi ushirikiano katika sekta ya biashara na sekta nyenginezo.

Dk. Mwinyi pia, alipongeza juhudi zinazochukuliwa na serikali ya Ethiopia katika kuiletea maendeleo nchi hiyo pamoja na wananchi wake.

Sambamba na hayo, Dk. Mwinyi alisisitiza haja kwa nchi za Afrika kuendelea kushirikiana katika kuendleza sekta mbali mbali za maendeleo.

Alisisitiza kwamba  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuendeleza ushirikiano na uhusiano uliopo kati ya pande mbili hizo.

Dk. Mwinyi alimpongeza balozi Sanbe kwa kumpa taarifa juu ya hali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii inavyoendelea nchini humo na hatua zinazochukuliwa na serikali ya Ethiopia katika kuhakikisha mafanikio yanapatikana.

Awali balozi wa  Ethiopia nchini Tanzania, Yonas Yosef Sanbe alimueleza Dk. Mwinyi kwamba uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Ethiopia ni wa kihistoria ambao umeasisiwa na hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na mfalme Haile Selassie.