NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wakandarasi wa mradi wa maji wa benki ya Exim kuelewa kuwa mradi huo unapaswa kukamilika kwa wakati.

Dk. Mwinyi alitoa muongozo huo jana alipotembelea mradi huo uliopo Dole, wilaya ya Magharibi ‘A’, ikiwa mwanzo wa ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo na kusikiliza changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi.

Alisema pamoja na mradi huo kuchelewa kuanza kwa wakati, umekuwa na kasoro na urasimu katika utekelezaji wake jambo ambalo linapaswa kuepukwa.

Alisema mradi huo unaogharimu zaidi ya dola milioni 92.18 ni wa miezi 18, hivyo ni lazima ukamilike kwa wakati na kukabidhiwa serikalini kwa muda uliopangwa.

Alisema sababu zote zilizotolewa kukwamisha hatua ya kuanza mradi huo, ni mambo yalio ndani ya uwezo wa watendaji wa mamlaka inayohusika.

Aidha, alitembelea visima vibovu eneo la Welezo na visima vya maji vilivyoko Bumbwisudi na kusema huduma za maji zipatikane ndani ya kipindi kifupi, kijacho kupitia njia ya muda mfupi na muda mrefu.

Alisema Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) itachukua hatua za kuweka mashine  mpya za kusukuma maji katika maeneo ambayo zimeharibika na kutengenza matangi ili maji yawafikie wananchi.

Aliutaka uongozi wa ZAWA kuwajibika na kuwa karibu na wananchi ili uweze kutatua changamoto mbali mbali ziliopo za ukosefu wa huduma hiyo muhimu kwa wananchi.

Nae, Mwakilishi wa Jimbo la Bububu, Mudrik Ramadhan Soraga, alisema mradi wa maji wa benki ya Exim ni muarubaini wa utatuzi wa changamoto ya ukosefu wa maji, sio tu kwa jimbo la Bububu, bali kwa wilaya za Magharib ‘A’, ‘B’ na wilaya ya Kati.

Soraga alibainisha umuhimu wa Serikali kuondokana na utaratibu wa kuwa na miradi mingi na kuchimba kisima kimoja kimoja na badala yake kuwa na mradi mmoja utakaohusisha uchimbaji wa visima vingi.

Aidha, Mkurugenzi Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Dk. Salha Mohamed Kassim alisema mradi wa maji wa benki ya Exim unalenga kuimarisha huduma za upatikanaji wa maji, unagharimu zaidi ya dola milioni 92.18, ikiwa ni fedha za mkopo kutoka benki ya nchini India.