Aliniamini, alikuwa kama mzee wangu
NA RAJAB MKASABA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema nia njema aliyokuwa nayo hayati Benjamin Mkapa ilichangia kupatikana kwa muafaka wa kwanza wa kisiasa Zanzibar.
Dk. Mwinyi alisema hayo jana katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam wakati akitoa hutuba kwenye maadhimisho ya kumbukizi ya Benjamin Mkapa, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali.
Alisema muafaka wa kwanza ulisaidia sana kutuliza joto la kisiasa Zanzibar na kufugua fursa za majadiliano na mashurikiano ya kisiasa katika visiwa hivyo vya Zanzibar.
Aliongeza kuwa msimamo wake juu ya muuungano ulikuwa thabiti, usiyoyumba na alikuwa tayari kuusimamia na kuulinda kwa kauli na vitendo.
Alisema hayati Mkapa aliifanyia nchi mambo mengi makubwa ya kiuchumi na soko ambayo yamekuwa na mchango mkubwa kwa Zanzibar na kuweza kuifungua kutoka katika ukiritimba wa uchumi wa karafuu.
Alifahamisha kuwa Zanzibar ni mnufaika mkubwa wa miradi ya taasisi ya Benjamin Mkapa tangu mwaka 2007 ambao miradi hiyo imejikita katika sekta ya afya hususan kujenga uwezo wa watumishi wa afya katika kutoa huduma zinazohusu UKIMWI, kifua kikuu, malaria na afya ya mama na mtoto.
“Tunajivunia mafanikio yaliyopatikana kupitia miradi hii ambayo imesaidia sana juhudi za serikali ya Mapinduzi ya Zanziar kutimiza wajibu wake wa kuhakikisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wote”, alisema Dk. Mwinyi.
Aidha, alisema anafarajika kwamba mazungumzo ya mashirikiano kati ya serikali anayoiongoza na taasisi ya Benjamin Mkapa yako katika hatua nzuri ambapo yakikamilika yatasaidia sana azma ya kupunguza uhaba wa watumishi wa sekta ya afya, na upatikanaji wa fedha za kuwezesha lengo la serikali anayoiongoza kumpatia bima ya afya kila Mzanzibari.