Awaonya wateule wanaojihusisha vitendo hivyo

Yaliyozungumzwa na wadau yanasikitisha sana

 NA KHAMISUU ABDALLAH

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema hatosita kumchukulia hatua mtendaji yoyote aliyemteuwa ambae atabainika kujihusisha na vitendo na vitendo vya udhalilishaji.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo katika kingamano la harakati za kutokomeza vitendo vya udhalilishaji Zanzibar lilojadili walipotoka, walipo na wanapokwenda lilofanyika katika ubumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.

Alisema haiwezekani yeye kama kiongozi anachukua juhudi za kupambana na matendo hayo huku baadhi ya watendaji wanakwamisha juhudi hizo na kubainisha kuwa inasikitisha kusikia viongozi aliowateuwa wanajihusisha na udhalilishaji

“Jambo linalonisikitisha sana kwamba wateuzi ninaowateua nao naambiwa wanahusiana na udhalilishaji niwaambie wananchi kwamba nimefanya kimakosa na nikibaini kwamba yupo mtendaji ambae anafanya mambo haya basi sitasita kumchukulia hatua,” alibainisha.

Hata hivyo, alisema anaendelea na dhamira yake ya kupambana na jambo hilo ili vitendo vya udhalilishaji wa kijisia vinaondoka nchini na kwamba wananchi waliotoa maoni katika kongamano hilo wameonesha taasisi zina jukumu la kupambana na vitendo hivyo.

Alisema umefika wakati kujipanga upya katika kupambana na matendo ya udhalilishaji nchini kwa ngazi zote zinazohusiana na kushughulikia mambo hayo.

“Ukiyasikia haya yanayosemwa hapa mimi binafsi napata huzuni kubwa kwa sababu inaonekana tasisi zinazotakiwa kufanya kazi zao hazifanyi na zina watu wanajulikana lakini wapo wanendelea kutizamwa bila ya kuchukuliwa hatua,” alisema.