NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha inavipatia maji safi na salama vitongoji sita vilivyomo katika shehia za Muungoni na Kitogani sio zaidi ya Julai 30, 2021.

Dk. Mwinyi ametoa agizo hilo jana wakati alipokitembelea kituo cha maji kilichopo Kitogani, ambapo pamoja na mambo mengine alitaka kufahamu changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo, ikiwa mwanzo wa ziara yake ya kuutembeela Mkoa Kusini Unguja.

Aliwataka watendaji wa Mamlaka hiyo kukamilisha mchakato wa kuvipatia huduma hiyo mapema iwezekanavyo kwa kukiwekea kituo hicho mundombinu kutoka mradi wa Ras al Khaimah wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni moja za maji kwa siku, sambamba na kukiwekea kituo hicho Paipu mpya ili kiweze kutoa huduma kwa ukamilifu.

Aliwataka viongozi wa ZAWA kuwajibika na kuwawajibisha watendaji wote wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, akibainisha kuwepo utendaji dhaifu wa watendaji katika mamlaka hiyo kwa kipindi kirefu.

Aliuagiza uongozi wa ZAWA kuhakikisha maeneo yote yanayomilikiwa na mamlaka hiyo, ikiwemo vituo vya maji yanapimwa na kupatiwa hati za umiliki.

Aidha, Dk. Mwinyi alisema serikali itayafanyia matengenzo majengo yote ya skuli, ili kuona kunakuwepo mazingira bora ya upatikanaji wa elimu nchini.

Akitembelea skuli ya sekondari Mtule, Dk. Mwinyi alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha ufaulu unaongezeka maskulini, hususan katika Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo taarifa zinabainisha kuwepo katika orodha ya skuli zinazofanya vibaya zaidi kitaifa.

Alitaka kuwepo mikakati maalum kuinua hali ya kielimu Mkoani humo, huku akiwataka wazazi kuunga mkono juhudi hizo.

Vile vile Dk. Mwinyi alipata fursa ya kuwatembelea Wajasiriamali wa Wilaya Kusini wanaozalisha bidhaa mbali mbali, hafla iliyofanyika katika kiwanja cha mpira Paje na kuwataka Wawakilishi wa Majimbo ya Wilaya hiyo kukaa pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo, kuona namna gani ya kuwasaidia wajasiriamali hao katika kuwapatia mafunzo pamoja na masoko ya kuuzia bidhaa zao.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alitembelea Chuo cha Amali Makunduchi na kuona maendeleo ya ujenzi wa Chuo hicho ulioshindwa kukamilishwa kwa takriban miaka minne sasa.

Alisema tatizo kubwa linaloliukabili ujenzi wa jengo hilo ni kutokuwepo kwa usimamizi imara, akibainisha miradi mingi ya Serikali huzorota kwa sababu za kuleana.

Aliutaka uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kufanya tathmini ya matengenezo yaliyofanyika, ili kujua thamani ya kazi iliyofanyika, ikiwa ni hatua ya kumbana mkandarasi wa ujenzi huo, na kuona hatua gani za kuchukua, ikiwemo kuilipa Serikali.

Alisema kituo hicho ni muhimu katika maendeleo ya nchi, kwa vile kinatarajiwa kutoa wataalamu  na kukidhi mahitaji  ya kiuchumi kupitia sekta ya uvuvi.

Aidha, Dk. Mwinyi alitembelea barabara ya Kiwengwa – Mtende yenye urefu wa kilomita 4.7, ambapo Serikali imepanga kuijenga kwa kiwango cha lami.

Alisema Serikali imetafakari na kuamua matengezo yote ya barabara za ndani zifanyike  kwa kiwango cha lami baada ya kubaini ujenzi wa barabara hizo kwa njia ya  kifusi kuwa hauna tija.

Alisema barabara za ndani zenye urefu wa kilomita 220 pamoja na barabara kuu zenye urefu wa kilomita 220 zote zitajengwa kwa kiwango cha lami, huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano ili kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo.

Vile vile Dk. Mwinyi alitembelea hospitali ya wilaya Makunduchi na kusema Serikali inalenga kuanzisha Hospitali zitakazoendana na hospitali husika pamoja na kuahidi kushughulikia maslahi ya wafanyakazi, ikiwemo mishahara na maposho kwa kadri ya uwezo wa Serikali utakavyoimarika, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha kunakuwepo utoaji bora wa huduma za afya nchini.

Naye, Mkurugenzi wa Mamlaka ya (ZAWA), Dk. Salha Mohamed Kassim alisema mipango ya ZAWA kwa mwaka wa fedha wa 2021 ni kupeleka miundombinu ya maji katika kituo kilichopo Kitogani kupitia mradi wa kisima cha Ras al Khaimah.

Alisema ongezeko la watu, sambamba na upungufu wa maji katika visima katika baadhi ya maeneo  ndio sababu ya kuwepo changamoto ya ukosefu wa huduma hiyo.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadidi Rashid, aliwasilisha taarifa za Utekelezaji wa shughuli za Maendeleo za Mkoa  wa Kusini, ambapo pamoja na mambo mengine  alieleza changamoto kadhaa zinazoukabili Mkoa huo, ikiwemo migogoro ya ardhi.

Alisema changamoto kubwa za migogoro ya Ardhi zinazoukabili Mkoa huo  zinatokana na sababu tofauti, ikiwemo kutokuwepo kwa hati ya matumizi ya ardhi, eneo moja kumilikiwa na watu zaidi ya mmoja pamoja na ukosefu wa ufahamu wa matumizi  sahihi ya eka tatu.