NA MWINYIMVUA NZUKWI

KUZUKA kwa maradhi ya Covid 19 ulimwenguni kumechangia kuwepo kwa matatizo ya mfumo wa chakula katika maeneo mengi ikiwemo Tanzania.

Miongoni mwa athari hizo ni pamoja na uhakika wa upatikanaji wa chakula katika jamii na ukuaji wa sekta zinazotoa huduma ikiwemo ya utalii.

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Dk. Soud Nahoda Hassan, alieleza hayo jana wakati akifungua kongamano la kujadili mfumo wa chakula lililofanyika katika Chuo cha utalii Maruhubi, mjini Unguja.

Alisema kuwepo kwa mfumo mzuri wa chakula kutachochea kwa kiasi kikubwa mabadiliko katika maendeleo ya mwanadamu hivyo kongamano hilo litahamasisha  kasi ya mabadiliko ya dunia kwenye uzalishaji, ulaji na fikra kuhusu chakula.

Aidha alisema fursa hiyo pia itasaidia kuandaa mwelekeo wa baadae wa mfumo wa chakula na kuongeza nguvu za pamoja za kufikia malengo yaliyokusudiwa kitaifa na kimataifa.

“Kongamano hili linataka wananchi kushiriki kutoa maoni ingawaje sio rahisi kuwafikia watu wote, hivyo uwepo wetu hapa leo ni fursa yenu ya kuwakilisha maoni ya wajasiriamali wengine waliobakia lakini pia watumiaji wa chakula,” alisema.

Dk. Nahoda alieleza kuwa kongamano hilo limekuja baada ya kuonekana kuwa kuna tatizo ambalo linaendelea kukua siku hadi siku yatokanayo na kutokuwepo kwa mfumo sahihi wa utumiaji wa chakula katika jamii  hivyo kupelekea kuwepo kwa matatizo ya afya yanayotokana na lishe duni, udumavu wa watoto, uzito hafifu na kupindukia na ukosefu wa damu kwa mama wajawazito na wanaonyonyesha.

Aidha alitoa angalizo kuwa mfumo wa chakula hauzungumzii uwepo wa mlo kamili bali unagusa pia afya za wanyama na mazao yake, afya ya mimea na mazao yake na  uchumi na uwezo wa kaya na sera mbalimbali.

Waziri huyo aliwataka washiriki wa kongamano hilo kutumia mbegu bora zinazostahamili ukame, maradhi na wadudu ili kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa, kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira na kuweka mipango shirikishi ya matumizi sahihi ya ardhi na rasilimali za misitu.