NA KHAMISUU ABDALLAH
KAMATI inayosimamia tuzo za umahiri wa uandishi wa habari Zanzibar imeeleza haja ya waandishi kuzingatia ubunifu na weledi katika kazi wanazoziwashilisha katika mashindano.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo inayoundwa na taasisi za habari Zanzibar, wakati wakitangaza msimu wa pili wa tuzo hizo kwa mwaka 2021/ 2022 kwa waandishi wa Zanzibar katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Kikwajuni Zanzibar.
Alieleza kuwa ili kazi iweze kushinda, kuna haja ya mwandishi kufanya kazi ya ziada na kwamba upo umuhimu wa kuzingatia misingi ya taaluma na matokeo ya kazi ya mwandishi.
Akitangaza tuzo zitakazoshindaniwa kwa msimu wa pili, Katibu wa kamati hiyo, Imane Osmond Duwe, alisema tuzo hizo zitatolewa kama ni sehemu ya kuthamini kazi zinazofanywa na wandishi wa habari nchini.
Alisema tuzo hizo ni mwendelezo wa tuzo zilizotolewa Mei 30, mwaka huu ambapo katika msimu wa pili zimeongezeka na kufikia 11 badala ya tano za awali.
Alizitaja tuzo hizo kuwa ni ya uandishi wa habari za uchumi wa buluu (tuzo ya Dk. Hussein Ali Mwinyi), tuzo ya uandishi wa habari za jinsia na udhalilishaji (tuzo ya Maryam Mwinyi) na tuzo ya uandishi wa habari za Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) inayobeba jina la tuzo ya Maalim Seif Sharif Hamad.
Imane alizitaja tuzo nyengine kuwa ni ya uandishi wa habari za rushwa na uhujumu wa uchumi (tuzo ya ZAECA), tuzo ya uandishi wa habari za kodi kwa maendeleo ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), tuzo za uandishi wa habari za michezo, uandishi wa habari za uwajibikaji, uandishi wa habari za afya, uandishi wa habari za utalii, uandishi wa habari za mazingira na uandisihi wa habari wa haki za watoto.
Aongeza kuwa habari zitakazowasilisha ziwe za uchunguzi ambazo zitakwenda kwa mfumo wa makala au habari za kawaida zilizoandikwa kwa upana ikiwa ni matokeo ya utafiti mpaka uliofanywa kuhusu masuala mbalimbali ya kisekta.
Akizungumzia vigezo vya kuzingatiwa wakati wa kuandaa au kuwasilisha kazi hizo, alisema ni pamoja na ubora wa kazi, umuhimu wa kuzingatia uwiano sawa na jinsia na vyanzo vingi vya habari.