CAIRO, MISRI
ENEO la pembe ya Afrika hususan nchi za ukanda wa mto Nile zinakabiliwa na hatari ya kuzuka vita na machafuko makubwa baada ya Ethiopia kuanza awamu ya pili ya kujaza maji katika bwawa la jipya la kuzalishia umeme la Renaissance.
Hatua hiyo ya Ethiopia kujaza maji katika bwawa hilo imesababisha rais wa Misri Abdel Fattah kutoa vitisho vya kuishambulia kijeshi Ethiopia akisema kuwa, Cairo ina jeshi lenye uwezo mkubwa.
Kwa mujibu wa taarifa Abdel Fattah al Sisi alitoa vitisho hivyo siku chache zilizopita wakati wa ufunguzi wa kituo cha baharini cha jeshi la Misri.
Awali Abdel Fattah al Sisi wa Misri alitishia kwamba Cairo itatoa jibu lisilotasawarika iwapo nchi yake itapata madhara kutokana na bwana la Renaissance linalojengwa na Ethiopia katika mto Nile.
Matamshi hayo ya rais wa Misri yamejibiwa na Mkurugenzi wa idara ya uhandisi katika wizara ya ulinzi ya Ethiopia ambaye alisema kuwa, nchi yake iko tayari kulilinda bwawa hilo dhidi ya hujuma yoyote ya jeshi la Misri.
Jenerali Buta Bachata Debele alisema kuwa Ethiopia imejitayarisha kukabiliana na hujuma yoyote ya adui inayotaka kuvuruga mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo na kusisitiza kuwa anatarajia kwamba mgogoro huo utatatuliwa kwa njia za amani.
Misri na Sudan zinasema ujenzi wa bwawa hilo ambalo umegharimu karibu dola bilioni nne, utapunguza maji ya nchi hizo na hivyo kuvuruga maisha ya mamilioni ya watu.
Ethiopia inasisitiza kuwa bwawa hilo litachochea maendeleo na ustawi nchini humo na katika nchi jirani, wakati Sudan na Misri zina wasiwasi kwamba mradi huo utapunguza kiwango cha maji ya nchi hizo katika Mto Nile.