TAKRIBAN wastani wa waislam milioni 2.5 hudhuru kwenye miji mitakatifu ya Makka na Medina iliyopo nchini Saudi Arabia kila mwaka kwa ajili ya kutekeleza ibada ya hijja ambayo ni nguzo ya tano na ya mwisho ya dini ya kiislam.

Hata hivyo, tangu mwaka jana na mwaka huu kwa sababu ya kuibuka kwa janga la maradhi ya corona, Saudi Arabia ikiwa miongoni mwa nchi zilizoathirika na ugonjwa huo, imepiga marufuku wageni kutoka nchi za nje kuingia nchini humo na kuruhusu idadi ndogo tu ya wenyeji kushiriki kwenye ibada hiyo.

Ibada ya hijja imefaridhiwa kutekelezwa na muislam mara moja katika maisha yake na huhitaji mtu kuwa mzima wa kimwili na mwenye uwezo wa kifedha ili kufanya ibada hiyo.

Hii ni mara ya pili kwa nchi ya Saudi Arabia kwa karibu miaka 90, inaweka historia ya kupiga marufuku raia wa kugeni kwenda kufanya hijja nchini humo.

Lakini kuna tofauti gani iliyopo kati ya Eid ul-Fitr na Eid ul-Adha?

Eid ul-Fitr, maana yake ni sikukuu ya kumaliza mfungo na husherekewa kuadhimisha mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Kwa kawaida siku hii huwa ni siku rasmi ya mapumziko katika mataifa mengi yenye waumini wengi wa kiislamu, hata hivyo idadi ya siku za mapumziko huwa tofauti katika nchi mbalimbali.

Waislamu huanza sherehe hizi kwa kukusanyika kwa maombi ya kila mwaka ambayo hufanyika muda mfupi baada ya machweo. Ni kawaida kuwaona waislamu wakikusanyika katika misikiti na viwanja vya wazi kwa ajili ya swala ya Eid.

Kabla ya ibada hiyo, huwa wanatoa sadaka kwa maskini ambayo huitwa zakat el fitri ambayo hizo zaka yenyewe nayo ni moja ya nguzo kuu katika dini ya kiislamu.

Ni kawaida kwa miji mikuu katika mataifa yenye waislamu wengi kupambwa sana na sherehe kubwa kuandaliwa, watoto kununuliwa nguo mpya na kupewa zawadi mbalimbali. Eid ul-Fitr huadhimishwa baada ya kuonekana kwa mwezi wa Shawwal.

Eid ul-Adha

Eid al-Adha, ndiyo sikukuu kuu zaidi ya kidini miongoni mwa waislamu kote duniani na pia huwa ni siku ya mapumziko mataifa mengi yenye waislamu.

Eid al-Adha maana yake ni sikukuu ya kuchinja, hutumiwa kukumbuka wakati nabii Ibrahim (A.S) alipotaka kumtoa kafara mwanawe Ismael alivyoamriwa na Allah, lakini akapewa kondoo na Mungu amtoe kafara badala yake.

Sikukuu ya Eid ul-Adha huadhimishwa kuanzia siku ya 10 baada ya kuonekana kwa mwezi wa Dhu al-Hijjah. Ibada ya Hajj kwenda Makka huanza siku mbili kabla ya Eid al-Adha na tarehe yake huthibitishwa baada ya kuoenakana kwa mwezi huo wa Dhu al-Hijjah.

Eid al-Adha ina majina mbalimbali katika mataifa ya kiislamu. Katika nchi kama za Nigeria na Morocco eid huyo hujulikana kama Eid el-Kabir, wakati nchini Senegal na Gambia hujulikana kama Tabaski.

Nchini Uturuki Eid ul-Adha, hujulikana kwa jina maarufu kama Kurban Bayrami, ambapo katika nchi za Indonesia, Malaysia na Singapore hujulikana kama Hari Raya Haji.

Nchini Iran hujulikana kama Eid è Qurbon na katika nchi za India, Bangladesh, na kwa Kiurdu hujulikana kama Bakr-Id or Qurbani Eid.

Katika sikukuu hiyo waislamu pia huvalia mavazi yao mazuri na ya kupendeza siku hii na huenda msikitini asubuhi mapema baada ya kuchomoza jua kwa jili ya swala maalum ambayo ni sunna.

Kwa sababu ni eid ya kuchinja waislam wengi hujiandaa kuchinja wanyama kama ngamia, ng’ombe, mbuzi au kondoo hali hiyo ni kukumbuka kitendo cha imani cha nabii Ibrahimu.

Mnyama baada ya kuchinjwa, nyama yake hugaiwa jamaa, majirani na maskini ili nao wafurahie siku hiyo ya eid.

Katika baadhi ya mataifa na miji hairuhusiwi watu kuwachinja wanyama nyumbani kwao na hivyo mchinjia hutumiwa. Waislamu pia hutoa pesa za hisani kipindi hicho kwa ajili ya sadaka.

Waislamu hutumia Eid ul-Adha kusherehekea utiifu kamili wa nabii Ibrahimu kwa amri ya Mungu na kuwakumbusha wenyewe kuwa tayari kutoa kafara chochote ili kutimiza maagizo ya Mungu.

Siku ya eid waislamu hasa katika kanda ya Afrika Mashariki baada ya kutoleana salamu hutakiana ‘Eid Mubarak’ kwa kiarabu maana yake ni “sherehe au sikukuu njema au yenye baraka”.

Salamu nyingine maarufu za kutakiana eid njema katika sikuu ya Eid ul-Adha ni pamoja na Ciid wanaagsan, ambayo hutumiwa na waislamu wa Somalia, Mutlu Bayramlar salamu hiyo hutumiwa na waislamu wa Uturuki.

Nchini Indonesia salamu ya kutakiana eid njema huambizana Selamat Idul Fitri – Indonesia, Brunei na Singapore hutakiana eid njema kwa kusema Selamat Hari Raya. Waislamu nchini Nigeria huepeana salamu za eid kwa kusema Barka da Sallah.