Ni muimbaji, mtunzi na muigizaji
 Aiomba serikali kuendelea kuwasaidia wasanii

NA ABOUD MAHMOUD

“HILO haliwezekani Na wala halitokua
Leo nakuelezeni Muache kunichungua
Msiingie shidani Haya nimejaaliwa
Kwani hasa jambo gani Mie lakulaumiwa
Kama ni mmoja wa mpenzi wa nyimbo za taarab basi ukisikia ubeti huo nina hakika utakua umeshajua hiyo ni nyimbo gani ambayo imeghaniwa na muimbaji gani na pia iliimbwa katika kikundi gani.

Laa kama hujajua basi hiyo ni moja ya beti ya nyimbo maarufu inayojulikana kwa jina la ‘Haya ni maumbile yangu’ ambayo imeghaniwa na msanii chiriku, Fatma Issa Juma akiwa na kundi maarufu la Culture Musical Club.

Msanii huyo amefanikiwa kujijengea jina kubwa katika ramani ya muziki wa taarab kutokana na namna ya uimbaji wake na sauti yake aliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu ya kumtoa nyoka pangoni pamoja na kipaji cha utunzi wa mashairi ya taarab.

Kutokana na kuimba nyimbo nyingi na nyengine alizitunga yeye mwenyewe,mwandishi wa makala hii alimfuata msanii huyo hadi nyumbani kwake katika mtaa wa Kwaalamsha na kuzungumza nae mambo mbali mbali.

Kwa umbile la nje Fatma ni mfupi mwenye umbile la wastani mwenye rangi nyeusi ya kung’ara, mcheshi na mpenda masihara kwa watu wa rika tofauti.
Nilipotaka kujua alianza kwenye masuala ya sanaa alisema:

“Kwa kweli sanaa mimi nimerithi kutoka kwa wazee wangu, mama yangu mzazi alikua msanii muigizaji katika kikundi cha Africa Social Light wakati huo kilikua maeneo ya Miti Ulaya”.

” Baba naye alikua muimbaji akiimba na marehemu Siti bint Saad na mimi mwenyewe nilianza tangu nikisoma madrasa nilikua naghani kasida na skuli nikiimba nyimbo za ngoma asili tulizokuwa tunacheza,”alisema.

Msanii huyo anasema sanaa yake aliianzia rasmi katika ngoma ya kidumbak huko alikuwa anaimba, anapiga pamoja na kucheza na kusema kwamba mpaka hivi sasa wakati akiwa anakwenda kwenye shughuli na ngoma hiyo ikipigwa anaimba.

Hamu ya kuwa msanii ilitawakali kwenye kichwa chake ambapo mwaka 1974, Fatma alijiunga rasmi na kundi la Culture Musical Club na kukutana na wasanii wengi mahiri akiwemo Rukia Ramadhan,Mwapombe Khiyari na marehemu Asha Simai.

Anasema, akiwa anajiunga na kundi hilo alikua akiimba nyimbo za marehemu Jabu Omar ikiwemo ‘Mola kampa kipaji’ Kuku asilaumiwe na nyengine nyingi ambapo anasema siku aliyotolewa kiukumbi aliimba nyimbo ya Rukia Ramadhani inayojulikana kwa jina la ‘Njoo mpenzi njoo’.

Anasema, mwaka 1975 alianza rasmi kuimba nyimbo zake mwenyewe zilizokuwa zikitungwa kwenye klabu hiyo zikiwemo zile za kuhamasisha chama na Serikali na baadae akanza kuimba nyimbo za kawaida ikiwemo ‘Maafa yamemfika’ Kiwewe na nyengine mbuzi isio na meno.

Anasema, mwaka 1983 aliondoka katika kikundi cha Kidongo Chekundu na kurudi katika kundi lake la Culture ambapo mara baada ya kufika hapo alitunga na kuimba nyimbo nyingi ikiwemo ‘Bughudha sitaki, wacha kujihashua na nyengine nyingi.

Msanii huyo aliondoka Culture mwaka 1986 na kuhamia katika kikundi cha jeshi huko pia alifanikiwa kutunga nyimbo nne ambapo nyimbo mbili aliziimba mwenyewe alizitaja nyimbo hizo ni pamoja na Nuru yangu na Nimesalitika.

Ilipofika mwaka 1990 alitoka kikundi cha jeshi na kuhamia katika kikundi cha ‘nyota zinazomeremeta’ ‘Twinkling Star’ kilichokua kinaongozwa na msanii nguli, Mohammed Elyas huko aliimba nyimbo moja inayojulikana kwa jina la ‘Ndoto njema’.

Mwaka 1994, msanii huyo alirejea nyumbani Culture ambapo huko alitunga nyimbo kadhaa zikiwemo ‘haya maumbile yangu na ‘kunionya sikatai’.

Moja ya beti ya nyimbo haya maumbile yangu ni kama ifuatavyo:-

“Asokasoro hakuna Aloumbwa na muweza
Mwenye lile hili hana Ndio shani yake Aza
Tabia kutolingana Si jambo la kushangaza
Kinachonikera sana Nisonalo kupakaza

Kiitikio

“Kunisema Sichukui
Kusengenya Haifai
Ni hekima Njema rai
Kunionya Sikatai”.

Kutokana na umahiri wake wa kuimba na kutunga, msanii huyo alichukuliwa na kundi la Tanzania One Theater(TOT) la jijini Dar es Salaam ambapo alisema akiwa katika kundi hilo alipewa nyimbo moja, lakini, akilataa kutokana na haikua na maadili na alidumu katika kundi hilo kwa muda miezi sita na baadae kurudi nyumbani Zanzibar.

“TOT sikuweza kudumu kwa sababu mambo yao na mimi tofauti hata nyimbo zao zilinishinda na ndio maana nikaamua kurudi nyumbani “.

“Na kipindi hicho kulikua na safari ya kwenda Ujerumani na uchaguzi mkuu wa 1995 ndiyo nikaamua kurudi hapo Culture na kazini kwangu Wizara ya Habari”, alisema.

Anasema, baadae Wizara ya Habari ilianzisha kikundi cha taarab kilichojuulikana kwa jina la ‘Sanaa Taarab mwaka 1998 na yeye alipewa uhamisho wa kuhamia huko.

“Baada ya kuanzishwa sanaa na mimi nikawa miongoni mwa viongozi ikanilazimu niachane na Culture kutokana na kuwa na majukumu mengi na kubakia na kikundi kimoja tu cha sanaa”.

Anasema, akiwa ndani ya sanaa taarab alifanikiwa kutunga nyimbo nyingi ambazo nyengine aliziimba mwenyewe na nyengine kuimba watu wengine miongoni mwa nyimbo hizo ni pamoja na ‘nenda utakako, tenda nawe usifiwe, ‘adui kiumbe, ‘umewashuka, ‘limbukeni hana siri, ‘yenu hamsemi, ‘ninavyokupenda na nyengine nyingi.

Beti ya nyimbo nnavyokupenda inasema hivi:-

“Mapenzi nikupendayo Shahidi wangu jalali
Sabili roho na moyo Na changu kiwiliwili
Natosheka unipayo Sitaki tena wapili
Nidhati nikwambiayo Sikama nakukejeli

Kiitikio
“Yao yasikushuli Ni wewe nilokuona
Moyo umekukubali Si leo wala si jana
Mimi wako sijidhili Kazi kwao walonuna”.

Baadae Fatma anasema, alikua anachukuliwa kwa mkataba katika vikundi mbali mbai kikiwemo kikundi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU ) huko aliimba nyimbo mbili na kikundi cha Magereza pia aliimba.

Nilipotaka kujua kwanini siku aliyoimba nyimbo ya ‘haya maumbile yangu alilia na alinijibu: “Kweli nililia na sikulia kama nilifanya makusudi, lakini kutokana na maneno niliyoyasema katika ile nyimbo nilijishtukia natokwa na machozi”.

Fatma anasema anavutiwa na uimbaji wa wasanii Mohammed Ilyas, Rukia Ramadhan,Sabah Muchacho, marehemu Asha Simai na marehemu, Bakari Abeid.
Kuhusu changamoto alizokumbana nazo msanii huyo anasema ni nyingi ikiwemo kuumwa kutokana na kazi yake ya usanii na mambo mengine ambayo anayakabili mwenyewe kuyatatua na kwa upande wa faida ni kuwa maarufu na kutembea nchi mbali mbali duniani.
“Changamoto zipo nyingi, sehemu mnayokuwa watu wengi kila mmoja ana tabia yake, lakini nashukuru naweza kukabiliana nazo na kuzitatua mwenyewe, lakini, faida ya kuwa maarufu na kutembea tu sina jengine,”.

“Naona tabu, nahangaika na sanaa naitangaza sanaa yangu halafu sina hata kibanda cha kujistiri nabakia kulalamika kila siku kazi yangu kukodi nafikiria nikifa wanangu hasa wanawake watakwenda wapi naiomba serikali na rais wetu anisaidie”, alisema kwa uchungu.

Kuhusu tofauti ya taarab asilia na taarab ya kisasa,msanii huyo anasema yeye anaona taarab asilia ndio taarab kwani inafunza mambo mbali mbali ambayo hata kama sio msanii, lakini, jamii kwa ujumla anatakiwa kuwa nayo.

“Taarab asilia ndio taarab imetufunza mambo mengi ambayo binadamu anatakiwa kuwa nayo imetufunza ukisimama jukwaani usalimie,imetufunza kuvaa nguo za heshima, nyimbo zinazoimbwa zenye maadili lakini saivi taarab ya kisasa hakuna hayo,”alisema.

Fatma alitoa wito kwa wasanii hususan wasanii wa kiume ambao wanakua viongozi waachane na tabia ya kutongoza wasanii alisema kufanya hivyo ndio kunakosababisha heshima katika sanaa na vikundi kwa ujumla kuondoka.

Mbali na fani ya uimbaji pia msanii huyo aliwahi kutunga michezo ya kuigiza aliyoipa majina ya ‘mkuki kwa nguruwe’ na ‘apizo la mke ambapo maigizo hayo yote yeye mwenyewe alishiriki kuigiza.

“Nawashauri viongozi wa wasanaa hasa wanaume tabia ya kuzoeana na wasanii wa kike na kuwa nao kimapenzi kunasababisha heshima kuondoka ili sanaa izidi kukua na irudi hadhi yake tufate mfumo ule ule wa zamani, lakini pia wasanii wadogo wakubali kufundishwa ikiwemo kuimba na hata katika maswala ya uvaaji wa nguo,”alisema.

Aidha, alitoa wito kwa taasisi ya haki miliki Zanzibar (COSOZA) kuzidisha bidii ya kuwasaidia wasanii katika kuzilinda kazi zao ambazo zinaibiwa na watu wasiowatakia mema wasanii.”Naipongeza sana COSOZA mana ipo mstari wa mbele kutetea haki zetu sisi wasanii na nawaomba wazidi kuongeza bidii kuwabana hawa wizi ambao wanatuibia kazi zetu sisi tukawa masikini wao wakatajirika kupitia kazi zetu,”alisema.

Bi Fatma Issa hivi sasa ana kikundi chake kinachojulikana kwa jina la ‘Wapendanao’ambapo anasema kinakabiliwa na ukosefu wa vyombo vya kupigia, lakini, tayari wameshatunga nyimbo zikiwemo za udhalilishaji.

Fatma Issa Juma alizaliwa Februari 2 mwaka 1957, Kianga wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja akiwa mtoto wa mwisho katika familia ya watoto watatu.
Elimu yake aliianzia mwaka 1962 kwa elimu ya Quran katika madrasa ya Mwalimu Mohammed Ali, Kibandahatari, mwaka 1965 alianza elimu kidunia katika Skuli ya Kidutani kuanzia darasa la 1-7 na baadae kuendelea na elimu ya Sekondari katika Skuli ya Haile Selassie.

Fatma amjaaliwa kupata watoto wanne, wawili wanaume na wawili wanawake ambapo katika watoto wake mmoja wao wa kiume anaitwa Hamdani ndiye aliyerithi fani ya sanaa ambae anatunga na kuimba nyimbo za dansa na taarab.

Anasema kuna nyimbo anatarajia kuimba inayoitwa ‘masikini wa bahati tajiri wa mikosi’ ambayo muziki umewekwa na Hamdani.

“Mwanangu Hamdani yeye ndiye karithi nyayo zangu, yeye anatunga mashairi ya taarab na dansa na pia anaweka muziki na mwanangu mkubwa, Saadun yeye yupo katika mchezo wa mpira wa miguu”.