NA MWANDISHI WETU

LEO ni siku ya Arafa ambayo ni kubwa na tukufu kwa waislamu, Siku hii ndiyo kilele cha ibada ya Hijja, na siku inayofuata ni siku ya Idil Adh’ha ambapo mahujaji huanza rasmi ibada ya kuchinja. Siku mbili hizi (siku ya Arafa na Idd Aldh’haa) zina hukumu na umahususi wake kwa kila Muislamu.

Leo hii waislamu wan chi mbalimbali duniani wamefunga ingawa sio faradhi na halizimishwi muislamu kufunga.

Arafa ni ile siku ya tisa tokea siku iliyoandama mwezi wa Dhul-Hijja duniani. Wanazuoni wamekubaliana kwamba, funga ya siku ya Arafa ndiyo funga bora mno katika siku za kufunga.

Kulifafanua hilo, Mtume wa Mungu (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) amesema: “Funga ya siku ya Arafa nataraji kwa Allah ifute dhambi za mwaka uliopita na ujao.” [Muslim]. Kifupi ni kwamba, funga ya siku ya Arafa inampadisha mtu daraja, inamuongezea mema na kufutiwa dhambi.

Ila, kwa kuzingatia kuwa funga za sunna zina fadhila kubwa mbele ya Allah. Mwenyezi Mungu anasema: “Na mkifunga ni bora kwenu, kama mnajua.” [Qur’an, 2:184]. Allah akasema tena“Rukuuni na msujudu, na muabuduni Mola wenu Mlezi, na tendeni mema, ili mfanikiwe.” [Qur’an, 22:77].

Kama inavyoeleweka kuwa kila mtu anahitaji kufanya mambo mema na mazuri kwa nia ya kujipendekeza (kujikurubisha) kwa Mwenyezi Mungu na kujiongezea thawabu na malipo kwani thawabu za Allah hazina mipaka.

Kwa kuzingatia hayo, inafaa kila Muislamu ajibidiishe katika kutenda amali nyingi za heri kwa kutaraji kupata moja ya mambo mawili; mosi, kujikurubisha kwa Allah na kutenda heri,

Bila shaka kila mwanadamu ni mkosa, na kwa kuwa kila mtu anakosea, Allah Mtukufu ametuletea ibada za wajibu na sunna ikiwamo funga ya Arafa kwa lengo la kuziba upungufu na kujiongezea ujira.

Kiujumla, funga ya siku ya Arafa ni sunna kwa wasiokuwa Hijja, na hii inatokana na ujira mkubwa wa kufutiwa dhambi za miaka miwili upatikanao katika siku hii.

Ama kwa mahujaji, wao si sunna kufunga siku hii ili mtu asamehewe ni sharti aache dhambi kubwa kama ilivyosemwa katika Aya hii: “Mkiziepuka dhambi kubwa mnazokatazwa, tutakufutieni makosa yenu madogo, na tutakuingizeni mahali patukufu.” [Qur’an, 4:31].  

Mtume wa Allah (rehema na amani ya Allah iwe juu yake): “Sala tano, na Ijumaa hadi Ijumaa, na Ramadhan hadi Ramadhan, ni kafara ya yaliyojiri kati yake, iwapo dhambi kubwa zitaepukwa.” [Muslim].

Ama kwa mtu anayefunga siku ya Arafa kwa sababu ya himizo la Mtume na kutekeleza sisitizo la kisharia, huyo haikatazwi kufunga katika siku iliyokatazwa, na kama atafunga siku moja kabla itakuwa bora.

Hapo, mtu atafunga siku moja kabla, kwa sababu kufunga siku moja baada (yaani siku ya Idd ya Adh’haa) haiwezekani. Kufunga siku ya Idd kisharia ni haramu kwa Waislamu wote (mahujaji na wasio mahujaji).

Kama Hadithi ya Abi Said (Allah amridhie) aliyesema: “Mtume amekataza kufunga siku mbili; Siku ya Idil fitri, na siku ya Idi Nnahri (ya kuchinja).” Katazo hili linamaanisha kwamba ni haramu kufunga swaumu ya aina yoyote katika siku zilizokatazwa.

Sambamba na hilo, katazo hili halimhusu Hujaji aliyenuia Hijja ya Tamatui na Qirani kisha akakosa mnyama wa kuchinja.

Huyu anaruhusiwa kufunga ndani ya siku kumi za Hijja kwani anatakiwa kufunga siku tatu ndani ya siku za Hijja na siku saba wakati atakaporejea nyumbani.