JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

WATU zaidi ya 72 wameuawa na zaidi ya watu 800 wamekamatwa katika ghasia zilizoanza kama maandamano wiki iliyopita ya kupinga kwenda jela kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Jacob Zuma.

Maduka na maghala nchini Afrika kusini yameporwa kwa siku ya tano mfululizo, licha ya hatua ya rais Cyril Ramaphosa kupeleka wanajeshi mitaani ili kuzima kudhibiti hali.

Waandamanaji waligeuza maandamano hayo na kuwa ghasia mwishoni mwa wiki, wakichoma moto, kufunga barabara kuu na kuvamia na kupora maduka.

Ghasia tayari zimesababisha uporaji mkubwa ukifanyika kwenye mji mkuu wa kiuchumi wa Johannesburg pamoja na jimbo la kusini mashariki la KwaZulu Natal.

Mzozo umezuka kwenye uwanja wa kisiasa, ambapo wapinzani wakuu wa Afrika Kusini wanawashtumu watu wenye msimamo mkali kwa kuchochea ghasia. Wanajeshi 2,500 wamepelekwa kusaidia polisi, waliokua wamezidiwa.

Lakini idadi hiyo ni ndogo sana ikilinganishwa na zaidi ya wanajeshi 70,000 waliopelekwa kwenye mitaa mwaka jana, ili kusaidia kuimarisha masharti makali ya kupambana na janga la corona.

Iidadi ndogo ya wanajeshi walionekana kwenye baadhi ya vituo vya biashara. Ghasia zilizuka kwa mara ya kwanza ijumaa iliyopita baada ya rais wa zamani Jacob Zuma kuanza kutumikia kifungo cha miezi 15 jela, hatia kudharau mahakama.

Mwishoni mwa juma, ghasia zilienea katika jimbo la Gauteng ambalo linajumuisha mji wa Johannesburg, ambako miili 10 ilipatikana Jumatatu kwenye kitongoji cha Soweto.