NA MWANDISHI WETU

KOCHA mkuu wa klabu ya Simba Didier Gomes, amemshukuru Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa hiyo, Mohamed Dewji (Mo) na Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez, kwa ushirikiano waliompa hadi kutetea ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara.

Gomes alisema uongozi wa klabu ukiongozwa na Mo na Barbara walimuamini na kumpa ushirikiano mkubwa, na ndiyo sababu iliyowafanya kutwaa ubingwa wakiwa na mechi mbili mkononi.

Alisema huwezi kuwa kocha bora bila kuwa na wachezaji bora hivyo, amekimwagia sifa kikosi chake kwa uimara wake huku akisema wamestahili kutwaa ubingwa kwa mara ya nne mfululizo.

Raia huyo wa Ufaransa alisema msimu huu wamekuwa bora na wamestahili kutwaa ubingwa, kwa sababu ndiyo timu iliyofunga mabao mengi na kufungwa machache kuliko zote.

“Lazima tumshukuru Mwenyekiti wa Bodi na CEO Barbara kwa ushirikiano walionipa, kwanza kuniamini naweza kuifundisha hii timu na kuipa mafanikio’.alisema

“Pia siwezi kuacha kuwataja wachezaji wangu kwenye ubingwa huu, huwezi kuwa kocha bora bila kuwa na wachezaji bora, pia tulikuwa na kikosi imara. Tumestahili kuwa mabingwa msimu tulikuwa bora zaidi ya timu zote,” aliongeza .