HATIMAYE aliyekuwa rais wa Afrika Kusini mzee Jocob Zuma amejisalimisha polisi kwa hiyari yake ili akatekeleze hukumu ya kifungo cha miezi 15 inayomkabili.

Polisi nchini Afrika Kusini imethibitisha kwamba Zuma alijisalimisha polisi baada ya wiki moja kupita tangu atiwe hatia ya kuidharau mahakama kufuatia kesi yake ya ufisadi na kuhukumiwa kifungo cha miezi 15 gerezani.

Usiku wa kuamkia jana ulikuwa wa kwanza wa maisha mapya gerezani kwa Jacob Zuma, ambaye atatumikia 15 kutokana na kutiwa hatiani kwa kuidharau mahakama.

Baada ya kufikiwa makubaliano ya kujisalimisha kwake na ujumbe wa polisi uliofika nyumbani kwake mapema juzi, Zuma alisindikizwa na walinzi wake alikwenda katika gereza lililokaribu na nyumbani kwake katika jimbo la KwaZulu Natal.

Dakika chache tu kabla ya muda wa mwisho aliopewa na mahakama kujisalimisha kwa hiari kabla ya polisi kumkamata, Zuma aliondoka nyumbani kwake Nkandla akisindikizwa na msafara wa magari.

Msemaji wa polisi Lirandzu Themba nchini Afrika Kusini alithibitisha katika taarifa kwamba Zuma yuko katika jela la polisi, kwa kufuatisha uamuzi wa mahakama ya katiba.

Polisi walipewa amri ya kumtia mbaroni hadi mwishoni mwa Julai 7 mwaka huu endapo atapinga kujisalimisha kwenda kutumikia kifungo chake.

Katika taarifa nyingine, mamlaka ya magereza imesema Zuma amefikishwa kwenye kituo cha mamlaka ya magereza, umbali wa kilomita 175 na makaazi yake ya mji wa Nkandla.

Baadhi ya wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika nje ya nyumba yake walielezea kutofurahishwa kutokana na hatua ya kiongozi huyo kujisalimisha mwenyewe na kwenda kutumikia kifungo chake.

Awali polisi ilitoa onyo la kutaka kumkamata rais huyo mstaafu mwenye umri wa miaka 79, iwapo hatajisalimisha mwenyewe, ifikapo usiku wa kuamkia juzi wangetumia nguvu.

Taasisi ya Zuma imeandika kwenye ukurusa wake wa Twitter “Zuma ameamua kutii amri ya kifungo, yuko njiani kujisalimisha kwa mamlaka ya magereza ya KwaZulu Natal.

Zuma ameamua kujisalimisha kwa mamlaka ili kutii agizo la mahakama ya katiba nchini humo iliyomkuta na hatia ya kudharau agizo la mahakama na kumpa adhabu ya kifungo cha miezi 15 jela.

Kabla ya Zuma kujisalimisha mahakamani kwenda kutumikia kifungo alisema hatojisalimisha na kuchukizwa na hukumu hiyo alioyoiita kuwa siyo ya haki dhidi yake.

“Hakuna haja ya mimi kwenda jela”, Zuma aliwaambia wanahabari siku ya nje ya makazi yake huko Nkandla katika jimbo la Kwa-Zulu Natal.

Alidai kwamba amepewa adhabu ya kwenda jela bila ya kusikilizwa na kudai kwamba Afrika Kusini inarejea kwa kasi katika utawala wa kibaguzi.

“Makabiliano mabaya yangetokea kama kama polisi wangejaribu kunikamata,” Jacob Zuma aliwaambia mamia ya wafuasi wake ambao walilipuka kwa miluzi na shangwe.

Mfuasi wake mmoja, Lindokuhle Maphalala, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa kama mkuu wa polisi angekuja kumkamata Zuma kwanza inabidi aanze na sisi.

Kabla ya kujisalimisha gerezani kulikuwa na mkusanyiko mkubwa wa wafuasi wake ambao ni haramu kwa kuwa unavunja kanuni za kudhibiti ugonjwa wa corona, lakini hakukuwa na askari waliokwenda kuwaondosha watu.

Aidha baadhi ya watu nchini humo walieleza kuwa Zuma kutokamatwa kwa  nguvu  kumefanya kuona kiongozi huyo yupo juu ya sheria kwa kuwa ana nguvu kubwa ya kisiasa.

Hata hivyo, mahakama ya juu zaidi nchini Afrika Kusini ilikubali kusikiliza ombi la Zuma la kutaka rufaa dhidi ya kifungo cha miezi 15 jela.

Taasisi ya Jacob Zuma, mfuko wa misaada wa rais wa zamani, ilisema rufaa dhidi ya amri ya kukamatwa itasikilizwa na mahakama kuu ya jimbo la KwaZulu-Natal.

Jacob Zuma mwenye umri wa miaka 79 aliondolewa mamlakani mnamo 2018, baada ya miaka tisa kutokana na kukabiliwa na shutuma za ufisadi.

Zuma amerudia kusema kuwa yeye ndiye muathiriwa wa njama za kisiasa akikataa mashitaka na pia anakataa kutoa ushirikiano katika uchunguzi juu ya makosa wakati wa uongozi wake.

Rais huyo wa zamani alitoa ushahidi mara moja tu wakati wa uchunguzi wa kile kilichojulikana kama kutekwa kwa serikali lakini akakataa kujitokeza tena baadaye.

Katika suala tofauti la kisheria, Zuma alikana shutuma zilizomkabili katika kesi yake ya ufisadi iliyohusisha makubaliano ya silaha ya thamani ya dola bilioni 5 kutoka miaka ya 1990.