NA KASSIM ABDI, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameipongeza Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kukamilisha vyema zoezi la uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana.

Hemed alieleza hayo jana wakati akipokea ripoti ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2020 iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud aliyeambatana na wajumbe tume hiyo waliofika ofisi kwake Vuga mjini Zanzibar.

Alisema ZEC imetekeleza vyema jukumu lake kwa weledi na umahiri kutokana na kuzingatia sheria zinavyowaelekeza jambo ambalo limesaidia wananchi kujenga imani dhidi ya watendaji wa tume hiyo.

Alifafanua kwamba kazi nzuri iliofanywa na watendaji ni ya kupigiwa mfano sambamba na kutoa ishara kwamba kupitia zoezi la uendeshaji wa uchaguzi nchi nyengine kutoka barani Afrika wanaweza kuja Zanzibar kujifunza namna bora ya kuendesha uchaguzi kuanzia hatua za awali za kuwaandikisha wapiga kura.

Aliwahakikishia kwamba yeye akiwa mtendaji mkuu wa shughuli za serikali ataendelea kutoa kila aina ya ushirikiano unaohitajika katika kufanikisha kazi za tume kutokana na Imani kubwa alionayo kwa viongozi wa tume.

“Mimi binafsi ni shuhuda wa kazi nzuri mliyoifanya naendelea kuwapongeza na kuwashukuru kwa kazi nzito kutokana na kulikamisha vyema jukumu mlilokabidhiwa na taifa”, alisema Hemed.

Alieleza licha ya changamoto zilizosababishwa na baadhi ya wanasiasa kutaka kuvuruga zoezi hilo lakini ubobezi na ufanisi wa watendaji wa tume wakiongozwa na makamishna, waliweza kuzikabili na kuzitatua changamoto hizo.

Akiwasilisha ripoti hiyo Mwenyekti ZEC, Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Tume imeamua kukabidhi ripoti kwake kwa kutambua kuwa Makamu wa Pili wa Rais ndiye kiongozi mkuu wa shughuli za serikali na kimuundo Tume hiyo ipo chini ya ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.