NA KASSIM ABDI, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amewagiza watendaji wa taasisi za serikali kuacha tabia ya kuwazungusha wawekezaji walioonesha nia ya kuwekeza Zanzibar ili kutoa fursa ya nchi kupiga hatua za kimaendeleo.

Hemed alitoa onyo hilo wakati alipofanya ziara ya kutembelea eneo linalojengwa kiwanda cha kutengeneza maji katika eneo la Chamanangwe wilaya ya Wete, mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema jambo la kuwazungusha wawekezaji walioonesha nia ya kuwekeza katika ardhi ya Zanzibar halikubaliki na serikali inayongozwa na Dk. Hussein Mwinyi haitolifumbia macho kwani kufanya hivyo kunalenga kurejesha nyuma azma ya serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Alieleza kuwa Zanzibar ilipoteza fursa siku zilizopita kwa kuwasumbua watu wenye nia ya kuwekeza katika maeneo mbali mbali kutokana na watendaji wa taasisi za serikali kuwasababishia usumbufu  wawekezaji hao.

Hemed alifafanua kwamba, endapo serikali itagundua  kuna taasisi inazorotesha kasi ya maendeleo ya serikali ya awamu ya nane basi hatua za haraka za kuwaondosha wasimamizi wa taasisi hizo zitachukuliwa.

Alieleza kuna faida nyingi zinazopatikana kutokana na uwekezaji huku akitolea mfano kutokana na uwekezaji inaisaidia serikali kukusanya kodi kwa ajili ya uendeshaji wa nchi sambamba na kutoa fursa za ajira kwa vijana.

Aligusia kuwa kuwepo kwa uwekezaji nchini pia kutaisaidia serikali kuweza kutatua changamoto za wananchi ikiwemo changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na Salama, Uhaba wa madawa pamoja na kukosekana kwa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika sekta ya elimu.

Nae, Muwekezaji anaejenga kiwanda cha Amos Industry Limited, Husamudin Ali Mussa, aliipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa jitihada zake kwa kuwapa kipaumbele wawekezaji kuwekeza jambo ambalo linatia moyo na wawekezaji wengi wameanza kujitokeza.

Alieleza kuwa, kiwanda hicho kitakapokamilika kitaanza uwekezaji wake kwa kutengeneza maji ya kunywa lakini baada ya muda mfupi kitajikita katika utengenezaji wa Juisi za matunda lakini malengo ya baadae wamekusudia kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mabati jambo ambalo litawapunguzia wananchi wake ghrama ya upatikanaji wa bidhaa mbali mbali.