Asema wamechangia uwepo wa amani, utulivu
Awataka kuendelea kutoa elimu, tahadhari ya Covid 19
NA KASSIM ABDI, OMPR
SEREKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk. Hussen Ali Mwinyi inathamini mchango unaotolewa na viongozi wa dini hali inayopelekea kudumisha amani na utulivu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo jana katika mkutano uliojadili nafasi ya viongozi wa dini katika kudumisha amani na utulivu uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakili, Kikwajuni jijini Zanzibar.
Hemed alisema mchango huo wa viongozi hao wanaoutoa kwa taifa umesaidia kwa kiasi kikubwa katika kustawisha maendeleo na kuchochea ustawi wa maisha ya wananchi.
Alieleza kuwa, uwepo wa amani na utulivu unaochangiwa na viongozi wa dini umesaidia kuwavutia wawekezaje tofauti jambo ambalo limepelekea kwa kupatikana kwa nafasi nyingi za ajira kwa jamii na kufanikisha kufikiwa kwa lengo la ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025.
Alisisitiza hali hiyo inapaswa kulindwa na kila mtu endapo kwani endapo ikipotea serekali na taifa kwa ujumla itashindwa kupokea watalii na wawekezaji hatimae kupunguza seheme kubwa ya Pato la Taifa.
“Nawaomba viongozi wa dini na wananchi wote kwa ujumla tuendelee kudumisha Amani na kila mmoja wetu aendelee kuwa mlinzi wa amani, utulivu na mshikamano wa nchi yetu” alisema Hemed.
Alifafanua kwamba, viongozi wa dini wamekuwa na moyo wa kijitolea katika kuhakikisha amani ya nchi inakuwepo muda wote kutokana na kazi nzuri walioifanya ya kuhakikisha amani kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Akizungumzia juu ya uwepo wa maradhi mbali mbali nchini, Makamu wa Pili wa Rais aliwapongeza viongozi hao kwa jitihada wanazozichukua katika kuelimisha waumini wanaowaongoza kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi ya covid – 19.
“Tumeshuhudia mchango mkubwa na mikutano mbali mbali mnayoifanya katika kupambana na maradhi ili kuhakikisha amani ya nchi hii haitetereki,” alieleza Makamu wa Pili wa Rais.