Asema kufanya hivyo kutaimarisha usalama wa watumiaji bahari
NA ASYA HASSAN
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, amesema serikali itaendelea kuchukua hatua kulipatia ufumbuzi suala la watu kuzama baharini ili kunusuru maisha yao.
Hemed alisema hayo katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohammed, katika maadhimisho ya siku ya kuzuia kuzama duniani.
Alisema Umoja wa Mataifa umepitisha azimio la kuadhimishwa kwa siku hiyo kutokana na ongezeko kubwa la matukio ya watu kuzama hususani katika nchi za uchumi wa chini na uchumi wa kati.
Aidha Hemed alifahamisha kwamba Zanzibar ni miongoni mwa nchi hizo hivyo serikali itaendelea kuliangalia kwa umakini suala hilo na kupatiwa ufumbuzi unaostahiki ili hatimae liweze kulizibitiwa kwa kiwango kikubwa au kulimaliza kabisa.
“Serikali inaitambua siku hii kutokana na umuhimu wake hivyo uwepo wake una uwezo mkubwa wa kuisaidia serikali na sekta binafsi katika kuchanganua, kupembua na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakumba wananchi hususani wanaotegemea kuendesha maisha yao kwenye sekta ya uchumi wa buluu,” alisema.
Mbali na hayo alisema serikali imekuwa ikichukua hatua ikiwemo kusimamia na kuliangalia kwa ukaribu zaidi suala hilo ili kupunguza matukio hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanasababisha kupoteza nguvu kazi ya nchi hususani katika maeneo ya kujitafutia kipato chao.
Alisema serikali imeandaa sera, kanuni na sheria na kujenga vituo na kununua vifaa vya uokozi ili kusaidia kukabiliana na tatizo hilo na kuwafanya wananchi kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mbali na hayo alitumia fursa hiyo kuishukuru taasisi ya Panje Project kwa kutoa mafunzo kwa walimu wa skuli nchini hatua itakayosaidia wanafunzi wengi ambao wataweza kuitumia taaluma hiyo katika nyanja na maeneo tofauti ili kusaidia kuepusha majanga ya kuzama kwa wananchi.