NA KASSIM ABDI, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambayo imelenga kuwainua wananchi kiuchumi.

Hemed alieleza hayo jana alipokuwa akizungumza na wadau wa maendeleo wanaoshughulikia masuala ya TASAF kutoka nchini Sweden waliofika ofisini kwake Vuga jijini Zanzibar.

Alisema serikali inaangalia uwezekano wa kuongeza nguvu katika sekta mbali mbali kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kupitia miradi ya TASAF, ambayo imeonesha muelekeo wa kupunguza umasikini miongoni mwa wananchi.

Makamu huyo alibainisha kwamba ujio wa ugeni huo utapata fursa nzuri ya kuitembelea miradi mbali mbali iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa ambayo imesimamiwa na viongozi wa TASAF hapa Zanzibar.

Alisema hatua ya ugeni huo kupata fursa ya kuitembelea miradi ya TASAF katika maeneo yaliyopitiwa na mradi huo, itathibitisha namna Zanzibar ilivyojipanga kuinua hali za maisha za wananchi.

Alisema miongoni mwa sekta watakazozitembelea ni pamoja na sekta ya afya na elimu ili kuona kwa jinsi gani miradi iliyotekelezwa imesaidia jamii sambamba na kushauriana juu ya namna bora ya kuweka vipaumbele kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mengine.