NA KASSIM ABDI, OMPR

MJUMBE wa Kamati Kuu ya halmashauri kuu ya CCM, Hemed Suleiman Abdulla amesema serikali ya Mapinduzi Zanzibar itawatatulia wananchi wakiwemo wa jimbo la Konde changamoto zote zinazowakabili.

Mjumbe huyo wa kamati kuu alieleza hayo katika mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Konde kisiwani Pemba unaotarajiwa kufanyika leo.

Hemed alisema katika kutekeleza ilani ya CCM, serikali imejipanga kutatua changamoto ndani ya jimbo hilo ikiwemo upatikanaji wa huduma za maji na matengenezo ya barabara za ndani kwa kiwango cha lami.

“Ndugu zangu wa jimbo Konde, serikali inayosimamiwa na Chama cha Mapinduzi imepanga kufanya mambo mazuri katika nchi hii ikiwemo katika jimbo hili, hivyo nakuombeni mpeni kura mgombea Sheha Mpemba awatumikieni”, alisema.

Alieleza Chama cha Mapinduzi tangu kimeanza kuzindua kampeni zake katika jimbo hilo imekuwa ikihimiza amani, utulivu na umoja kutokana na kuamini kuwa uwepo wa vitu hivyo ndio msingi wa kupatikana maendeleo.

Akiomba kura kwa wananchi wa jimbo hilo, mgombea wa nafasi ya ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi, Sheha Mpemba Faki aliwataka wananchi kubadilisha fikra na mtazamo ili waweze kujikomboa.

Alisema kwa miaka kadhaa watu waliowaamini na kuwapa nafasi ya kuliongoza jimbo hilo kutoka vyama vyengine wameshindwa kuwaletea maendeleo.

Akigusia sekta ya elimu mgombea huyo aliwaahidi wananchi kwamba endapo atapata ridhaa ya kuchaguliwa atahakikisha anapunguza matokeo mabaya ya mitihani ya kitaifa katika skuli za sekondari.

Alisema yeye ni mdau wa elimu, hivyo anajisikia vibaya sana kuwaona wanafunzi wanaishi kwenye kupata matokeo mbaya yasiyowapeleka kwenye njia ya kuzifikia ndoto zao.

Alisisitiza kwamba katika kampeni zake alifanikiwa kuwafikia takribani makundi yote yaliyokuwemo ndani ya jimbo hilo jambo linalotoa sura nzuri ya mafanikio kutokana na wengi wa wapiga kura aliowafikia wameonesha kuridhika nae pamoja na kumuunga mkono.

Naye, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kaskazini Pemba, alimhakikishia mjumbe huyo wa kamati kuwa akiwa yeye ni mwenye dhamana ya mkoa huo kichama atahakikisha jimbo hilo kupitia uchaguzi huo wa mbunge linachukuliwa na Chama cha Mapinduzi.

Kufuatia uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika leo Chama cha Mapinduzi kimevitaka vyama vyengine vya upinzani vilivyosimamisha wagombea kuwa wastaarabu kwa kukubali matokeo ya uchaguzi mara baada ya kutangazwa na Tume ya Taifa.