NA MWANDISHI WETU

MABADILIKO katika sehemu yoyote ile ni muhimu sana iwe kwa Serikali, taasisi ya umma ama ya binafsi au wakati mwengine hata nyumbani.

Kwa mantiki hiyo basi anaeongoza yoyote ni lazima kujikukubalisha kukosolewa na kupokea ushauri kutoka kwa anaowaongoza ikiwa na lengo la kuleta mabadiliko ya haraka kwenye sehemu anayoiongoza.

Rais wetu wa awamu ya nane Dk. Hussein Ali Mwinyi, daima katika hotuba yake amekuwa akihimiza namna ya uwajibikaji wa wafanyakazi katika sehemu zao za kazi.

Sambamba na hilo amekuwa akihimiza namna ya viongozi kuwa tayari kutatua kero za wananchi na pia watendaji wao wa chini kwa lengo la kuleta ufanisi katika kazi.

Dk. Hussein amebaini kwamba baadhi ya viongozi wamekuwa na viburi na jazba na kuwakosesha haki zao watendaji wa chini bila ya kueleza sababu za msingi jambo ambalo linaleta taasiwra mbaya sehemu za kazi.

Ni ukweli usiopingika kuwa ile kauli ya Dk. Hussein ya kuwa wako baadhi ya watu wanatafuta huduma sehemu za umma kwa siku, wiki, miezi n ahata miaka jambo ambalo linawezekana kupata siku moja tu, lakini kutokana na ubinafsi inachukuwa muda huo.

Hivyo Rais Dk. Hussein alisema katika utawala wake hatopendelea kuona hali hiyo ya watu kuhangaishwa na kukosa haki zao kwa uzembe wa mtu mmoja tu.

Sambamba na hilo hivi karibuni Rais Dk. Hussein alifanya ziara ya kikazi ya kuangalia utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo katika mikoa mitatu ya Unguja hasa katika kipindi chake cha uongozi.

Lakini katika ziara yake hiyo kulibainika mambo mengi ya ovyo ambayo baadhi ya miradi au huduma inahitaji fedha kidogo tu lakini haikutekelezwa kutokana na utashi wa mtu au kikundi cha mtu jambo ambalo linaonesha dhahiri kuwa watendaji hawatekelezi wajibu wao sehemu hasa wanaoziongoza.

Inashangaza sana kuona kuwa viongozi wanasubiri kupangiwa kazi na Ikulu kama anavyosema yeye mwenyewe Rais Dk. Hussein jamboa mbalo haliingia akilini kabisa na hivyo kukwamisha huduma kwa jamii huku nyengine zikiwa na umuhimu wa kipekee katika maisha ya binadamu hasa masuala ya afya.