SEHEMU kubwa ya watanzania ilikuwa na hamu ya kuwaona viongozi wakiwa mfano wa kutekeleza yale wanayoyazungumza dhidi ya wananchi katika maeneo mbalimbali.
Pamoja na mijadala mingi inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, mmoja wapo unaoendelea na uliochukua sehemu kubwa ni suala chanjo ya ugonjwa wa corona.
Ugonjwa huu umekuwepo kwa takriban mwaka mmoja na nusu na kiukweli umekuwa tishio kubwa hasa ikizingatiwa kuwa umepoteza maisha ya baadhi ya wapendwa wetu wakiwemo ndugu na jamaa zetu.
Wataalamu wamefanikiwa kuupatia chanjo ambapo kampuni kutoka nchi mbalimbali kwa sasa zinazalisha chanjo hizo na wananchi kwa mamilioni katika nchi nyingi ulimwenguni wameshapatia chanjo ya ugonjwa huo.
Baada ya kuingia madarakani kuingoza Tanzania kama rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan aliahidi kuongoza mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona ambapo aliunda tume iliyotoa mapendekezo juu ya namna ya kuudhibiti ugonjwa huo.
Katika mapendekezo ya tume hiyo ilishauri serikali ya Tanzania kuridhia kuingiza chanjo watakazopatiwa wananchi katika kuukabili ugonjwa huo unaosambaa kwa kasi.
Serikali ya Tanzania imeridhia kuingizwa kwa chanjo za ugonjwa wa corona na kupatiwa wananchi, ambapo zoezi rasmi ya uzinduzi wa chanjo hiyo limeanza ikulu ya Dar es Salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan.
Macho ya watanzania siku ya uzinduzi yalielekezwa kwenye vituo vya televisheni kumuona mama huyo wa taifa akidungwa sindano ya chanjo ya corona na mtaalamu wa afya pamoja na viongozi wengine wa ngazi ya juu serikalini.
Kwa hakika Samia ameonesha mfano na amekuwa kiigizo kikubwa kama kiongozi kwa watanzania kwa kuwaonesha na kuwathibitishia wananchi kuwa chanjo hizo hazina madhara kiafya na ni salama kwani wapo baadhi ya watu wanapotosha.
Inashangaza kuona wapo baadhi ya watanzania hata hawana utaalamu wowote wa afya, wanajaribu kujenga hoja ya kupinga chanjo, kukataza na kuwahamaisha wananchi wasijitokeze kuchanjwa corona.
Huwa tunajiuliza mara mbilimbili hivi hawa watanzania wenzetu wanaopinga na kuwahamaisha wananchi wasijitokeze kuchanjwa wana akili timamu? Na je hatua hiyo wanayoichukua ina faida gani kwao?
Tunauliza hivyo kwa sababu chanjo ni sala la hiyari, hivyo kama hupendi usijitokeze kwenda kuchanjwa, lakini huna haki ya kuwatisha wala wale wanaojali afya zao na wenye nia ya kuchanja.
Unaweza kutumia vyombo vya habari na mitandoa ya kijamii kuwasilisha hoja ya chanjo mjadala huo unaweza kuwa na faida kwa wananchi lakini sio kutoaa maamuzi kwa kuwaambia wasijitokeze.
Hivi kama rais wa amejitokeza hadharani mbele ya watanzania kwenda kufanya chanjo, tuseme hapendi maisha yake? Tuseme amechoka kuishi? Haogopi madhara?
Watazania tuache kuwa waongeaji sana, tusikubali turejeshwe nyuma na wale wanaotaka Tanzania daima iwe nyuma, dunia iko mbali twende nayo sambamba.
Chanjo ni jambo la hiyari ukifika wakati jitokeze ili uwe salama dhidi ya corona na ili ujikinge na uwakinge wengine. Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete aliwahi kusema “akili za kuambiwa changanya na zao”.