SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji (IOM), limesema idadi ya wahamiaji na wakimbizi waliokufa wakati wakijaribu kuingia Ulaya kupitia baharini, imeongezeka mara mbili kwa mwaka huu ikilinganishwa na miezi sita ya kwanza ya mwaka 2020.

Hayo yamebainishwa katika ripoti iliyotolwa na shirika hilo ambapo limesema takribani wahamiaji 1,146 wamekufa kati ya mwezi Januari na Juni mwaka huu.

Aidha IOM imesema idadi ya watu wanaosafiri kwenda Ulaya kupitia baharini pia imeongezeka kwa asilimia 56, ambapo njia kuu ya Bahari ya Meditaranea kati ya Libya na Italia ndiyo iliyosababisha vifo zaidi, ambapo watu 741 walikufa.

Watu 250 walikufa kupitia njia ya Bahari ya Atlantiki kati ya Afrika Magharibi na Visiwa vya Canary vilivyopo Uhispania, ambapo watu wapatao 149 walikufa kupitia njia ya eneo la Magharibi la Bahari ya Meditaranea kuingia Uhispania.

IOM ilisema kuwa mashirika yanayotoa msaada kwa shughuli za uokoaji wa raia yameendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali, na boti zao nyingi zimekwama katika bandari za Ulaya kutokana na kesi za jinai dhidi ya wafanyakazi wa boti hizo.

IOM pia inabainisha kuwa ongezeko la vifo linakuja wakati ambapo vizuizi vya boti zinazobeba wahamiaji kutoka pwani ya Afrika Kaskazini vinaongezeka.