NA HAFSA GOLO

SERIKALI imeombwa kuanzisha sheria ya ufugaji wa mbwa Zanzibar, ili kudhibiti maradhi ya kichaa cha mbwa ambayo yameonekana kuendelea kuleta athari kwa wananchi na kuambukiza wanyama wengine.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Maabara wa Mifugo kutoka Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar, Mohamed Abrahmani, alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Maruhubi kufuatia maradhi ya kichaa cha mbwa.

Alisema tatizo la maradhi ya kichaa cha mbwa bado lipo Zanzibar, hasa  maeneo ya Magharibi ‘A’ katika kisiwa cha Unguja.

Aidha alisema kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na maabara hiyo , kati ya wanyama 10 waliochunguzwa watano wamegundulika kuwa wanauguwa maradhi ya kichaa cha mbwa.

Mkuu huyo alitaja miongoni mwa wanyama waliogunduliwa  kuuguwa maradhi hayo ni pamoja na paka wawili.

“Kesi za maradhi hayo nyengine zimejitokeza maeneo ya Kigunda, Nungwi, Chukwani, Bambi, Chwaka na Kianga”,alisema.

Hata hivyo, alisema iwapo kutakuwa na sheria ya ufugaji wa mbwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kuweka mifumo mizuri kwa wafugaji ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mbwa wao wanapatiwa chanjo kila mwezi pamoja na tiba nyengine husika.

“Nchi nyingi duniani  zimekuwa na sheria ya ufugaji wa mbwa na zimeweza kufanikiwa katika udhibiti wa maradhi ya kichaa cha mbwa hivyo kuanzishwa kwa Zanzibar haitokuwa kiroja wala jambo geni”,alisema.

Nae Msaidizi Mkuu wa maabara ya Mifogo, Fatma Waziri akitilia mkazo juu ya uanzishwaji wa sheria hiyo alisema,wakati umefika serikali wa kuweka sheria na kanuni madhubuti zinazoendana na mahitaji ya sasa ili ziweze kusaidia changamoto ya maradhi hayo ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara nchini.