LONDON, England
ITALIA wamefanikiwa kufuzu fainali ya michuano ya Euro 2020 kufuatia kuifunga Hispania katika mikwaju ya penalti 4–2, baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya goli 1-1.
Mchezo huo wa nusu fainali ulipigwa kwenye dimba la Wembley jijini London.

Kiungo, Federico Chiesa, aliipa Italia goli la kuongoza kunako dakika ya 60, lakini, mshambuliaji Alvaro Morata, akaisawazishia Hispania kwenye dakika ya 80 akimalizia pasi murua ya Dani Olmo.

Italia sasa wanafikisha mechi 33 bila ya kupoteza chini ya kocha, Roberto Mancini.
Kwenye mikwaju ya penalti, Alvaro Morata, alipoteza na kuifanya Hispania itolewe kwa mara ya kwanza kwenye nusu fainali kwa mikwaju huku kiungo mkabaji wa Chelsea, Jorginho, akiibeba Italia.
Italia imekuwa na kiwango bora kwenye michuano hiyo kuanzia hatua ya makundi wakiwa wameshinda mechi 13 katika 33 pamoja na kufuzu kucheza fainali.

Hispania ilikuwa ikitafuta ubingwa wa tatu wa Ulaya baada ya michuano minne iliyopita wakati Italia imeshinda michuano hiyo mara moja, mara ya mwisho ikiwa ni mwaka 1968.
Italia na Hispania zimekutana mara 10 katika michuano mikubwa, huku Italia ikishinda mara nyingi zaidi hadi Hispania ilipowafunga kwa mikwaju ya penalti katika mechi za kuingia Euro 2008 kabla ya kuifunga Italia 4-0 katika fainali miaka minne baadaye.(BBC Sports).