TOKYO, Japan
IVORY Coast imefuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya soka ya wanaume kufuatia sare ya goli 1-1 na Ujerumani kwenye siku ya tano ya Olimpiki ya Tokyo.
Sare hiyo imeifanya Ivory Coast kumaliza nafasi ya pili kutoka kundi ‘D’ wakati wapinzani wao wametupwa nje ya michuano hiyo.

Ivory Coast iliongoza wakati Benjamin Henrichs alipojifunga kwenye dakika ya 67 alipowekwa chini ya shinikizo na Youssouf Dao.

Lakini, shuti la mpira wa adhabu ndogo lililopigwa na Eduard Lowen, liliifanya Ujerumani kusawazisha zikiwa zimesalia dakika sita kabla ya pambano hilo kukamilika.
Miamba hiyo ya Afrika sasa itamsubiri mpinzani wake kwenye hatua hiyo ya robo fainali baada ya kukamilika kwa ‘droo’ inayotarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi.

Wawakilishi hao wa Afrika walikuwa na akina Franck Kessie wa AC Milan, Max Gradel mwenye makazi ya Uturuki na Eric Bailly wa Manchester United kama wachezaji waliozidi umri.

Katika michezo yao mengine, Ivory Coast iliifunga Saudi Arabia magoli 2-1 na kutoka sare 0-0 na Brazil ambayo ilimaliza kinara wa kundi ‘D’.
Matokeo mengine ya mechi za jana, Saudi Arabia 1 vs Brazil 3, Korea Kusini 6 vs Honduras 0 na Romania 0 vs New Zealand 0.(BBC Sports).