NA MADINA ISSA

JAJI Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, amemuapisha Jaji Aziza Iddi Sued, kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kuu Zanzibar.

Hafla ya kiapo hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mahakama hiyo Vuga Mjini Unguja ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mahakama akiwemo Mrajisi wa Mahakama kuu ya Zanzibar.

Akizungumza mara baada ya kumuapisha, Jaji Makungu, alisema ni vyema watumishi wa Mahakama kuendelea kumpa ushirikiano wa kutosha, ili kazi ziweze kufanyika kama ilivyokusudiwa ikiwemo upatikanaji wa haki za watumishi.

Alisema, ushrikiano katika kazi unasababisha kuwepo kwa ufanisi katika kazi na kuweza kuleta mabadiliko katika utendaji wa kazi.

Nae, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Aziza Iddi Suedi, alisema atahakikisha kufanya kazi kwa mujibu wa sheria iliyopo ili haki za watumishi ziweze kupatikana.

Aidha aliahidi kushirikiana na watendaji wa tume na kuahidi kutofanya kazi kwa upendeleo na kuwataka kuendelea kufanya kazi, ili kuleta mabadiliko ndani ya taasisi.

Uteuzi huo ulifanyika mara baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania.