NA MWASHUNGI TAHIR, MAELEZO
JAJI Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, amewataka mahakimu kufanya kazi zao kwa uadilifu ili kuondokana na malalamiko ya wananchi katika sehemu zao za kazi.
Makungu alitoa wito huo jana wakati alipokuwa akiwaapisha Mahakimu Haroub Amour Bakari na Hidaya Muhamed Mussa kuwa wasuluhishi na waamuzi katika kitengo cha usuluhishi wa migogoro chini ya Kamisheni ya Kazi.
Hafla ya kuwapisha mahakimu hao ilifanyika katika ukumbi wa mahakama kuu Vuga na kusema kiapo hicho kimefanywa chini ya kanuni ya 11 namba 5 ya usuluhishi na uamuzi kanuni za mwaka 2011.
Alisema kuapishwa kwa wasuluhishi na waamuzi hao, kumeongeza idadi ya wasuluhishi na waamuzi katika shughuli za kazi na ni matarajio yake kwamba kazi hiyo itakwenda vizuri.
Vile vile Jaji Makungu aliwataka mahakimu hao kuacha upendeleo katika sehemu zao za kazi na kujitahidi kutekeleza majukumu yanayowakabili kwa ufanisi.
“Natamani kuona mnakwenda kuondosha malalamiko ya wananchi kwa haraka ili kuondokana na mrundikano wa malalamiko yanayohusu masuala ya kazi,” alieleza jaji Makungu.
Hata hivyo aliwasisitiza watendaji wa kamisheni hiyo kufanya kazi kwa mashirikiano na kuwatakia mafanikio mema kwenye utekelezaji wa kazi zao za kila siku ikiwa ni pamoja na kuepukana na migogoro.