PORT-AU-PRINCE, HAITI

POLISI nchini Haiti imetangaza kuwa, jaji wa zamani wa Mahakama Kuu ya nchi hiyo alihusika katika mauaji ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Jovenel Moïse.

Taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa ya Polisi ya Haiti ilisema kuwa, jaji wa zamani wa Mahakama Kuu anatuhumiwa kuhusika katika mauaji ya Rais Jovenel Moïse na kwamba jaji huyo alikutana na mamluki wa Kicolombia wanaotuhumiwa kutekeleza mauaji hayo.

Ripoti zinasema Polisi ya Haiti tayari imetoa kibali cha kutiwa nguvuni jaji wa zamani wa Mahakama Kuu ya nchi hiyo, Windelle Coq Thelot ambaye awali alikuwa ametuhumiwa kuhusika na jaribio la kufanya mapinduzi dhidi ya Rais Moise. Haijulikani jaji huyo amejificha wapi.

Mapema mwezi huu televisheni ya CNN ya Marekani imeripoti kuwa, Mmarekani wa tatu anayeshukiwa kuhusika na mauaji ya rais wa Haiti ametiwa nguvuni na vyombo vya usalama.

Ripoti ya CNN imenukuu duru za kuaminika kwamba, kundi la wauaji wa aliyekuwa rais wa Haiti, Jovenel Moïse, limethibitisha taarifa za kuhusika Marekani katika mauaji hayo.

Polisi nchini Haiti pia imetangaza kuwa imemkamata daktari mwenye uhusiano na Marekani ambaye wanaamini ndiye mpangaji mkuu operesheni ya mauaji ya wiki iliyopita ya Rais Jovenel Moïse wa nchi hiyo.

Bw Moïse, 53, aliuawa nyumbani kwake mnamo Julai 7 na mamluki 28 wa kigeni.Mkewe wake, Martine Moïse, alijeruhiwa katika shambulio hilo na kupelekwa hospitali kwa matibabu. Martine Moïse baadaye alielezea namna wauaji walivyoommiminia risasi mumewe katikati ya usiku.