NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali amesema amefanya mazungumzo ya ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo la Mitaji (UNCDF), ili kusaidia kupitia upya mfumo wa miundombinu ya sekta ya maji na kuondosha upotevu.

Hayo aliyasema jana, katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Uratibu wa Shughuli za SMZ, Dar es Salaam, wakati akifanya mazungumzo ya kiongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo la Mitaji (UNCDF), Peter Malika.

Katika mazungumzo yao waziri huyo alisema amekubaliana na kiongozi huyo kukutana katika kipindi cha wiki mbili kwa ajili ya majadiliano na utekelezaji wa miradi mbali mbali itakayoleta maendeleo kwa wazanzibari.

Alisema katika mazungumzo hayo wamekubaliana kuangalia maeneo ya ujenzi wa vituo vya daladala na masoko, ambayo bado kunaonekana kuna changamoto ya masuala hayo katika halmashauri na manispaa na pamoja na kupitia mifumo ya huduma ya maji ili kudhibiti upotevu wa maji.

Aliliomba shirika la UNCDF, kusaidia kuimarisha miundombinu ya sekta ya maji ili kuzuia upotevu mkubwa wa maji unaoendelea kwa sasa pamoja na kujengewa uwezo wa ukusanyaji wa mapato yanayotokana na huduma hiyo nchini.

Alifafanua kuwa upotevu wa maji ni mkubwa, ambapo ukipita maeneo mbali mbali ya mijini utakuta mabomba yamepasuka na kumwaga maji ovyo ovyo, hali ambayo inachangia kupotea huduma hiyo, na kuikosesha Mamlaka mapato.

Alisema sekta ya maji ni eneo muhimu la kuboresha miundombinu yake pamoja na kuweka mifumo mizuri ya udhibiti mapato yake, ambapo alisisitiza Mamlaka ya Maji –ZAWA inakabiliwa na changamoto kubwa ya kupotea kwa mapato wakati wa ukusanyaji.

“Tumeshuhudia mara kadhaa watu wanapelekewa bili wakati huduma hiyo hawana na kusababisha malalamiko na wakati mwengine watu wanatumia maji, lakini bili zao hawazipati hivyo kuna haja ya kuwekwa kwa mita za kisasa za kusoma matumizi ya huduma hii kwa wananchi”, alisema.