NA MWANDISHI WETU

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar katika kukabiliana na mripuko wa ugonjwa wa corona, imeanza kuchukua hatua kadhaa kuhakikisha inakabiliana na wimbi la tatu la ugonjwa wa corona.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto imezitaka taasisi mbali mbali kuendelea kuchukua tahadhari za kinga dhidi ya ugonjwa wa COVID 19.

Kama inavyoeleweka wakati huu dunia ikishuhudia wimbi la tatu la maradhi hayo,hivyo ni vyema wananchi wakaendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo kwani kuna uwezekano wa kulikumba Zanzibar kutokana na kuendelea kupokea wageni kutoka nchi mbali mbali ulimwenguni.

Ili tuweze kulitekeleza hilo, uongozi wa hospitali kuu ya Mnazi mmoja umeamua kuweka utaratibu unaowataka wananchi wanaoingia humo kuvaa barakoa wakati wote wakiwa katika mazingira ya hospitali.

Sambamba na hilo, lakini pia watoa huduma wote wa wagonjwa ni lazima  kuvaa barakoa ili kujikinga wao na wagonjwa dhidi ya maradhi hayo.

Hapana budi wananchi na jamii kwa ujumla kuunga mkono maagizo hayo kwa kuwa ugonjwa huu hauchagui hasa kwa kuwa huambukizwa kwa mfumo wa hewa.

Kwa kuwa ugonjwa huu si mgeni tena hapa Zanzibar hivyo tufuate utaratibu uliowekwa kama ulivyokuwa awali mara tu baada ya mripuko wa awali kuyafuata masharti yote kwa maslahi ya afya ya jamii.

Miongoni mwa maagizo hayo ni pamoja na kurudisha utamaduni wa kunawa mikono kwa kutumia sabuni na maji ya kutiririka ambayo yapo katika maeneo mbali mbali ya hospitali hiyo kama moja ya tahadhari.

Aidha wananchi hasa wale wanaofika mahospitali kwa ajili ya kuwaangalia wagonjwa wao ni lazima kuepuka mikusanyiko katika maeneo ya hospitali jambo ambalo litaepusha kuenea kwa haraka ugonjwa huo.