NA MWAJUMA JUMA
KWANZA kabisa nianze kutoa pongezi za dhati kwa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) kwa kukamilisha mchakato mzima wa uchaguzi na kupatikana rais mpya.

Aidha, nampongeza mshindi wa uchaguzi huo Abdul-latif Ali kwa kupata nafasi hiyo katika uchaguzi huo ijapokuwa ulikuwa mgumu, lakini, uliendeshwa kwa misingi ya uhuru na haki.
Lakini pia niipongeze kamati ya kusimamia uchaguzi ya ZFF kwa kuendesha uchaguzi huo kwa uwazi na kupatikana mshindi ambae ataliongoza shirikisho hilo kwa kipindi cha miaka miwili iliyobakia.

Baada ya kutanguliza pongezi hiyo sasa niingie katika historia ya chagunzi mbali mbali zilizofanyika katika shirikisho hilo katika vipindi vifu vifupi.
Itakumbukwa kwamba tokea kujiuzulu kwa aliyekuwa rais wa shirikisho hilo ambalo zamani ilikuwa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kumeshafanyika chaguzi mbali mbali na viongozi ambao wanashinda wanaishia kujiuzulu.

Marehemu Ali Ferej Tamim aliyeongoza ZFA kwa zaidi ya miaka 20 mpaka pale Juni 30, 2012, alipojiuzulu na nafasi hiyo kujazwa na Amani Ibrahim Makungu ambae aliongoza kwa miezi minane na kujuzulu.
Historia inaonyesha karibu marais wote hao wametoka madarakani baada ya wao wenyewe kujiuzulu na sio kushindwa katika uchaguzi.

Ravia Idarous Faina naye aliongoza shirikisho hilo na baadae kujiuzulu na kuja Seif Kombo Pandu ambae pia alijiuzulu Februari 17 mwaka 2021, huku sababu kubwa ya kujiuzulu huko kulichangiwa na kuwepo kwa migogoro ndani ya shirikisho hilo.

Soka letu kwa sasa limekumbwa na changamoto nyingi ambalo ukiliangalia linakosa haiba na sifa ikilinganishwa nan chi nyengine za Afrika Mashariki.Zanzibar katika miaka ya nyuma ilisifika kwa kuwa na viwango bora vya wanamichezo ambao walitamba katika Afrika Mashariki na Kati.

Hata hivyo kwa sasa soka hilo limekuwa ni la mwisho licha ya kuwa kuna vipaji vingi vya vijana lakini havionekani kutokana na kutawaliwa na ubinafsi pamoja na migogoro isiyokwisha.

Zanzibar tunashiriki mashindano mbali mbali ya mpira wa miguu, ikiwemo ligi za vijana, wanawake, ligi kanda ya Unguja, na ligi kuu lakini zote zimekosa mvuto kutokana na mambo ambayo yanafanyika kila kukicha.

Hivyo, matarajio yetu kwa rais huyu ni kuona mabadiliko makubwa katika soka letu.
Rais huyu ambae alichaguliwa kwa kupata kura 16 na kumpita mpinzani wake Suleiman Shaaban kwa kura nane, tunatarajia atakuwa rais muelewa na mweledi katika uongozi wake.

Pamoja na kuwa ni rais kijana na mdogo lakini ni matarajio kwamba ligi zetu zitarejea kuwa na msisimko kama ambavyo zilivyokuwa hapo zamani.

Kwa sasa tumeshguhudia ligi zetu zikichezwa pasipo na udhamini wala ufadhili kulikotokana na wadau wengi kutokuwa na imani na uongozi uliokuwepo lakini ni imani kwamba kwa rais huyu mambo yote yatakaa sawa na kufunguka.

Ufadhili na udhamini katika michezo ni mambo ya msingi ambavyo vinachangia vijana wetu kupata hamasa ya kushiriki katika michezo.Imekuwa aibu kuona ligi kuu inamalizika na bingwa anaondoka akiwa na kikombe na medali jambo ambalo linapaswa kukaliwa kitako na kuweza kulitafutia ufumbuzi.

Hivyo rais huyu anapaswa mbali na kuondoa migogoro tu katika soka letu lakini pia inampasa kuangalia kwa kiasi gani anafanikiwa katika suala zima la kupatikana kwa wafadhili katika ligi zao hasa ligi kuu.

Kitu cha msingi ambacho kitatakiwa kufanyika kwa rais huyu ni kujaribu kuondosha makundi na kujenga ushirikiano wa pamoja baina yao viongozi pamoja na wadau wa mchezo huo.

Mchezo wa mpira wa miguu unapendwa sana na unamashabiki wengi ambao wananekana wamerudi nyuma kutokana na kukosa ushirikiano.Hivyo rais huyu ajaribu kukaa pamoja na wachezaji wa zamani na wadau ili kufikia makubaliano ya ni njia gani itumike ili safari yao ya kuendeleza soka la Zanzibar inafikia pahala panapostahiki.

Jambo jengine la kufanyika awe karibu pia na waandishi wa habari ambao na wao wana mchango mkubwa katika kufanikisha safari hiyo.Hata hivyo juhudi za pamoja zinahitajika katika kuona tunajenga nyumba ya pamoja ili kuweza kulifikisha salama soka letu.
Aidha ujio wa rais huyo tuna matumaini kwamba utafunguwa ukurasa mpya katika soka la Zanzibar kwa ngazi zote.