MOMBASA, KENYA

GAVANA wa Mombasa, Hassan Joho huenda akakabiliwa na kifungo cha siku 60 jela endapo atashindwa kulipa faini ya shilingi za Kenya 250,000 kama ilivyoamuliwa na mahakama.

Mwanasiasa huyo mashuhuri atakabiliana na kifungo endapo atakashindwa kulipa faini hiyo iliyotolewa mahakamani kwa kubomoa ukuta wenye thamani ya shilingi za Kenya milioni mbili wa mwanabiashara Ashok Doshi mnamo mwaka 2019, kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa gazeti la The Standard, idhini ya kukamatwa kwa kiongozi huyo ilitolewa Mei 27, 2021, baada ya kupatikana na hatia ya kudharau mahakama mnamo Mei 21, 2021, inatazamiwa kutekelezwa na kamanda wa polisi kaunti ya Mombasa, Stephen Matu.

Mwakilishi Wadi wa Changamwe, Bernard Ogutu ambaye pia alishtakiwa pamoja na Joho pia alitarajiwa kufungwa jela kwa siku 14 ama alipe faini ya shilingi 20,000, ambayo tayari amelipa.

Wakili wa Doshi, Willis Oluga alimuandikia barua Matu akitaka Joho akamatwe ndani ya siku 14 kama alivyoamuru Jaji Sila Munyao mnamo Mei.

“Sasa tunawasilisha kwako amri na idhini iliyotolewa Mei 27, 2021 ya kumkamata Ali Hassan Joho ambaye ni gavana wa kaunti ya Mombasa na kumpeleka katika Gereza la Shimo La Tewa hadi athibitishe alilipa faini,” ilisoma sehemu ya barua ya Oluga.

Gavana Joho pia alipatikana na hatia ya kupuuza mahakama na kumtaka alipe faini ya kuharibu mali ya Doshi.