NA KHAMISUU ABDALLAH

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeelekeza uchumi wake katika sekta ya uchumi wa buluu ili kufanikiwa kama zilivyofanikiwa nchi nyengine duniani.

Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo wakati akizindua kitabu cha rais mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo cha THE ASIAN ASPIRATION hafla iliyofanyika jana katika hoteli ya Verde iliyopo Mtoni mjini Unguja.

Alisema umefika wakati Zanzibar kufanikiwa kama nchi yengine katika bara la Asia kwa kujipanga kwenye uzalishaji kupitia sekta ya uchumi za buluu ambao chanzo chake ni rasilimali ya bahari.

Alisema serikali imeweka mikakati kwenye sekta hiyo ili kuhakikisha jinsi zitakavyotumika fursa za bahari kwenye uvuvi na kukuza uchumi wa Zanzibar. “Tumejipanga kuwekeza kwenye bahari tukiamini kwamba itakuwa chachu ya kukuza uchumi wetu wa nchi yetu,” alisema.

Alibainisha kuwa nchi kama Japan imefanikiwa katika kukuza uchumi wake kwa kushirikiana na taasisi binafsi kwa kutumia teknolojia na kutengeneza gari ya TOYOTA na kuwa maarufu hapa Zanzibar.

Dk. Mwinyi alifurahishwa kuona kwamba changamoto nyingi zimetatuliwa nchini Nigeria na kuona umuhimu wake mkubwa katika kilimo ambacho kimekuza uchumi wa nchi na sekta ya utalii.

Akizungumzia kitabu hicho, Mwinyi alisema kwa bara la Asia kitabu hicho kimeweza kuonyesha maeneo katika bara la Afrika na inatagemea viongozi wengi wanahitaji kufanyiakazi bila ya mazoea ili kifikia malengo yao na kitabu hicho iwe ni chachu ya maendeleo ya Zanzibar.

Aidha alisema jina hilo linavutia sana kwa watu wa njanja tofauti kuanzia wachumi, viongozi wa kisiasa na hata wanaopenda kusoma vitabu.

Sambamba na hayo, alisema anaamini kwamba kitabu hicho kitakuwa na umuhimu kwa nchi za Bara la Afrika kuweza kujifunza mambo mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Zanzibar.