KINSHASA, DRC

JESHI  la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limetangaza kuwa, limefanikiwa kuwaokoa raia zaidi 150 waliokuwa wametekwa na kundi la waasi wa ADF mashariki mwa nchi hiyo.

Msemaji wa Jeshi kwenye mkoa wa Ituri Jules Ngongo aliwaambia waandishi wa habari kwamba, miongoni mwa watu hao waliokolewa ni pamoja na wanawake, wazee na watoto.

Aidha alisema hatua hii iliwezekana baada ya wanajeshi wa Serikali kuwazidi nguvu waasi hao wa ADF katika mapambano yaliyotokea kati ya Julai 18 na 20, katika maeneo ya Boga na Tchabi katika mji wa Irumu.

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limesema kuwa, raia hao waliotekwa, walikuwa wanatumiwa kama ngao na waasi hao wa ADF wakati wa makabiliano na maofisa wa usalama.

Ongezeko la mashambulizi ya magenge yenye silaha na machafuko ya kikabila yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 300 tangu mwanzoni mwa mwaka huu huku wanajeshi wa serikali na walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakijaribu kuleta utulivu mashariki mwa nchi hiyo bila mafanikio.

Mauaji hayo ya hivi karibuni yalitokea Beni, makao makuu ya Kivu Kaskazini licha ya Serikali kutangaza kulizingira jimbo hilo.

Tangu mwanzoni mwa mwezi wa Aprili, wakaazi wa miji ya Beni na Butembo huko Kivu Kaskazini wamekuwa wakiandamana kulaani mauaji ya waasi wa ADF.