NA JUMA KHATIB SHAALI

JAMII imeshauriwa kuzitumia kambi za Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), ili waweze kujifunza mbinu za uzalishaji wa kilimo cha mbogamboga kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.

Wito huo, ulitolewa na Mkuu wa Kikosi cha JKU Bambi Matola, Kapteni Suleiman Benjamin Simon wakati wa uvunaji wa zao la Pilipili Boga hapo katika kambi ya JKU Bambi Matola Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema kutokana na mahitaji ya mazao ya mboga mboga kisiwani Zanzibar, JKU iliweka utaratibu maalumu wa kutoa elimu ya uzalishaji wa mazao hayo kwa lengo la kupata mazao yenye ubora zaidi.

Kwa upande wake Bwanashamba wa kikosi hicho Sajenti Ramadhan Juma Ramadhan, alisema kutokana na mabadiliko ya Tabia ya Nchi, ni vyema jamii ikatumia mbinu za kisasa za umwagiliaji maji ili waweze kuzalisha zaidi.

Aidha, alifafanua kuwa jumla ya Ekari moja na nusu ya pilipili boga itavunwa ambazo zitatumika kama shamba darasa kwa wananchi pamoja na vijana wa kujenga Taifa na zinatarajiwa kuuzwa zaidi ya Shilingi milioni ishirini na mbili.

Akizungumza kwa niaba ya vijana wa kujenga Taifa, Hamad Iddi Mtondo, alisema wamefaidika na elimu wanayoipata kutoka JKU kwani wamefanikiwa kujifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kilimo, Ufugaji, Uvuvi pamoja na uzalendo wa nchi yao.

Hivyo aliwataka wazazi na walezi kuwapeleka vijana wao JKU ili kuweza kujifunza stadi mbali mbali za kazi na kuondokana na utegemezi kutoka kwa wazazi wao.