BUJUMBURA, BURUNDI

CHAMA kikuu cha upinzani nchini Burundi, CNL cha Agathon Rwasa, kimelazimika kupaza sauti baada ya mmoja wa makada wake kutekwa nyara wiki iliyopita.

Élie Ngomirakiza, mkuu wa chama hicho katika wilaya ya Mutimbuzi mkoa wa Bujumbura alikamatwa na wanajeshi wakiwa kwenye gari la kijeshi lililotambuliwa na mashahidi, chama hicho kinabaini.

Inaelezwa kuwa takriban majira ya saa 10 mchana, Élie Ngomirakiza, mkuu wa chama cha CNL katika wilaya ya Mutimbuzi, kaskazini magharibi mwa Bujumbura, alikuwa aanapeleka matofali kwa mteja wake ndipo alipowasili kwenye lango la mji mkuu wa kiuchumi wa Burundi, Bujumbura, gari lake lilisimamishwa na gari la jeshi.

“Kulingana na habari tuliyonayo, kulikuwa na askari kwenye gari, pia nambari za usajili wa gari hilo zinajulikana ni A031,” alisema msemaji wa chama cha CNL, Thérence Manirambona, huku akiongeza kuwa gari hilo ni la ofisa wa jeshi.

Baadhi ya mashahidi waliokuwepo wakati wa tukio hilo wanadai kuwa waliweza kuwatambuwa baadhi ya watu waliokuemo katika gari hilo aina ya ‘4X4’ ya jeshi la Burundi, ambaye ni Luteni-Kanali Aaron Ndayishimiye anayeongoza kikosi cha 212 kinachopiga kambi katika msitu wa Rukoko, karibu na mpaka na DRC huku maafisa wawili wa utawala katika eneo hilo ambao walimuonyeshea kidole kada huyo wa chama cha CNL kwa askari ambao walimteka nyara.

Aidha Chama cha CNL kimeomba uchunguzi ili kubaini mazingira halisi ya kutoweka kwake.Hata hivyo bado hakuna taasisi ambayo imethibitisha au kukanusha madai ya chama hicho, iwe utawala, polisi, jeshi au hata Tume ya kitaifa ya haki za binadamu (CNIDH).

“Ofisi zetu zinaendelea kuharibiwa, hii inaonyesha kuwa hakuna uvumilivu wa kisiasa tunaomba vitendo hivi vya unyama visikomeshwe ”alisema Thérence Manirambona.