NA HAROUB HUSSEIN

UBALOZI wa Tanzania nchini China umepokea shehena ya chanjo za maradhi ya Covid 19 zilizokabidhiwa wiki iliyopita kwa niaba ya Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar.

Chanjo hizo zilizotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ikiwa ni kutimiza ahadi yake iliyoitoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi karibuni.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu, Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, alisema amepokea chanjo hiyo aina ya Sinovac ambayo imeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Aidha Balozi Kairuki aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa msaada huo ambao alisema utasaidia jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukabiliana na maradhi hayo.

Hivyo alitoa rai kwa wananchi watakaopenda kuchanja kutumia fursa hiyo ya kujikinga na ugonjwa kwa kuchanja pamoja na kuchukua tahadhari zinazotolewa na Wizara ya Afya katika kujikinga na maradhi hayo.

Kairuki alisema msaada huo wa chanjo walizozipokea unatarajiwa kusafirishwa kutoka China Julai 30, mwaka huu na unatarajiwa kufika Zanzibar siku hiyo hiyo.

Wiki mbili zilizopita, Balozi Mdogo wa China Shang Shisceng, aliyepo Zanzibar, alikabidhi hati za msaada huo kwa Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, ofisini kwake Vuga ili kuongeza nguvu ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.