NA MWANDISHI WETU
KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imekutana katika kikao maalumu, Ikulu Jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka, alisema hayo katika taarifa yake aliyoitoa kwa vymbo vya habari nchini Tanzania.
Alisema Kamati Kuu imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuruhusu chanjo ya virusi vya ugonjwa wa korona (UVIKO 19) Kutolewa nchini, na yeye kuwa mfano wa kukubali kuchanjwa ikiwa ni udhibitisho wa usalama wa chanjo hiyo.
Alisema uamuzi wake ni kielelezo cha upendo na uzalendo mkubwa alionao katika kujali afya za watanzania na ni hatua nzuri ya Tanzania kuungana na dunia katika kukabiliana dhidi ya UVIKO-19,
Alisema hatua hiyo pia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025 Ibara ya 83(o) na 84.
Kamati Kuu alisema imeelekeza kuanza kuchukuliwa hatua kwa wale wote wanaokiuka mienendo, taratibu na kanuni za maadili na uongozi kwa mujibu wa katiba ya Chama Cha Mapinduzi.
Aidha Kamati Kuu imefanya uteuzi wa makatibu wakuu wa Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi, ambapo Gilbert Kalima Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania na Dk. Philis Nyimbi Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT).