NA MWANDISHI WETU, KARAGWE 

CHAMA cha Ushirika cha Wilaya za Karagwe na Kyerwa (KDCU) imeongeza tija ya uzalishaji wa kahawa kufuatia kupata soko la uhakika la soko la kimataifa kwa zao la kahawa kutoka kwenye wilaya za Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera.

Akiongea na wanahabari, Meneja Mkuu wa KDCU, Oscar Mujuni, amesema kuongezeka kwa tija na soko la kimataifa kwa zao la kahawa kutoka kwenye wilaya hizo hasa baada ya kufanyika kwa marekebisho mbalimbali kwenye mchakato mzima wa kilimo unaozingatia ubora wa kahawa inayozalishwa.

Mujuni amesema kuwa wamefanikiwa kupata wanunuzi hao kufuatia uamuzi wa kuzingatia ubora wa zao hilo hali iliyongeza imani ya wanunuzi wa kahawa duniani ambao sasa wanaagiza kiasi kikubwa zaidi cha kahawa kutoka Tanzania.

“KDCU imefanikiwa kupata wanunuzi wa kahawa kutoka nchi za Ulaya ikiwemo, Uswizi, Uingereza na Ufaransa hali inayoongeza tija ya uzalishaji kwa wanachama wa ushirika huo,” alisema.

Kwa mujibu wa Mujuni, uzalishaji na uchakataji wa zao la kahawa mkoani Kagera umepunguza kwa kiasi kikubwa ukosefu wa ajira kwa kuongeza idadi kubwa ya maelfu ya watu wanaojiajiri au kuajiriwa kwenye kilimo cha zao hilo wakiwamo vijana, akinamama na hata wazee, hali ambayo imewaongezea kipato na kuinua kiwango cha mahitaji yao.

Mujuni amelinganisha uboreshaji wa sasa wa zao la kahawa na miaka ya nyuma kwa kutoa mfano wa mwaka 2017, wakati ambao kahawa iliyozalishwa wakati huo iliuzwa na maganda yake ikiwa haina thamani kubwa huku ikiwa inauzwa kwa mtu yeyote yule, kukiwa hakuna taarifa za ziada endapo kahawa ilikuwa inafika kwenye soko la kahawa la kimataifa.