NA JOSEPH NGILISHO ARUSHA
MKE wa malalamikaji katika shauri namba 87/2020 la wizi wa shilingi milioni 300 ,Fridah Emmanuel (51) Mkazi wa Njiro jijini Arusha, ameiambia mahakama kuwa hakumwona mshtakiwa , Joel Kazimoto, ambaye ni mfanyakazi wao wa Ndani akiiba kiasi hicho Cha fedha zilizokuwa ameficha kwenye nguo zake za ndani katika kabati la nguo chumbani
Shahidi huyo, watano kwa upande wa mashtaka katika shauri hilo lililofunguliwa na mume, Emanuel Wado (Sunda) ambaye ni mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa hotel ya kitalii ya Mt. Meru, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki, Mbele ya hakimu , Pamela Meena wa mahakama ya hakimu Mkazi Arusha, wakati akihojiwa na wakili wa utetezi , Edmund Ngemela ambaye anamtetea mshtakiwa Joel Kazimoto.
Awali akiongozwa na wakili wa serikali Grace Medikenya alieleza kuwa siku ya tukio Disemba 12 ,2019, alitoka nyumbani kwake majira ya asubuhi na baadaye kurejea saa nane mchana.
Alisema alipofika na kuingia ndani chumbani kwake na kukuta baadhi ya nguo zake za ndani zikiwa chini na kumuuliza msichana wake wa kazi aitwaye Scolla iwapo mume wake (Emmanuel Wado) kama alirudi nyumbani mchana na kujibiwa kwamba hakurudi.
Alisema wakati akitafakari alisikia muungurumo wa pikipiki aliyodai ni ya Joel, ukitoka nyumba kwake ,alijaribu kumpigia simu, lakini hakupokea.
Alisema aliendelea kuangalia mazingira ya chumbani kwake ndipo alipobaini kwamba dirisha la chuma (Grill) katika chumba hicho lilikuwa limefunguliwa na kuwekwa chini na ndipo alipopata picha kwamba kwamba Joel ndio alikuwa akiwaibia.
Alisema kuwa matukio ya wizi katika chumba wanachoishi yeye na mumewe yalianza kutokea Kati ya Aprili mwaka 2018 na Disemba 2019.
Ambapo Aprili ,2018 zilipotea kiasi cha dola 7000 na simu ya mikononi zilizokuwa kwenye kabati la nguo za Ndani.
Aliendelea kuieleza mahakama hiyo kwamba mnamo June 2018, yalipotea madini aina ya Tanzanite yenye thamani ya milioni 200 yaliyokuwa yamefungwa na kuwekwa katika kabati hilo la nguo katika chumba Chao.
Alisema Agosti 2019, kiasi cha shilingi milioni 60 zilizokuwa ndani ya kabati katika chumba chake zilipotea katika mazingira ya kutatanisha.